TAMBO, mbwembwe na kejeli zilizokuwa
zikitolewa kwenye mikutano ya kampeni za kuwania ubunge wa Chalinze leo
zinatarajia kufikia kikomo wakati wakazi wa jimbo hilo watakapopiga kura
Wagombea watano kutoka vyama vya CCM,
CHADEMA, CUF, NRA na AFP ndio
watakaomenyana kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wagombea hao ni Mathayo Torongey
(CHADEMA), Phabian Skauki wa (CUF), Vuniru Hussein (NRA), Ramadhani Mgaya (AFP)
pamoja na Ridhiwani Kikwete (CCM).
Uchaguzi huo unafanyika kutokana na
kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo, kufariki Januari 22,
mwaka huu.
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Samuel Salianga, alisema vituo
vitakavyotumika kupigia kura ni 288 na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ni
92,939.
Salianga alisema maandalizi ya
uchaguzi huo yamekamilika kwa asilimia 95 na tayari vifaa vyote muhimu
vimeshafika na kusambazwa katika vituo vya kupigia kura.
Alibainisha kwamba vituo
vitakavyotumika ni vile vilivyotumika katika uchaguzi uliofanyika katika mwaka
Uchaguzi Mkuu 2010.
Dk. Slaa afunga kampeni
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod
Slaa, jana alifunga kampeni za kuwania ubunge wa Chalinze kwa kuwaomba wananchi
wamchague mgombea ubunge wake, Mathayo Torongey.
Dk. Slaa, alisemaTorongey
akichaguliwa ataongeza nguvu ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye
kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwakilisha masilahi na
matakwa ya wananchi.
Aliwataka wasikichague Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na mgombea wake, kwani kufanya hivyo ni ‘kuhalalisha’ kuwa
wanakubaliana na hali ngumu inayoikabili nchi, ikiwemo ugumu wa maisha na
ufisadi unaotishia amani ya nchi.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa
ufungaji wa kampeni hizo uliofanyika jana Chalinze mjini, kwenye Uwanja wa
Masoko, Slaa alisema uchaguzi huo mdogo ni fursa ya kudhihirisha nguvu ya
wanyonge dhidi ya watawala.
Alisema kuwa matatizo ya huduma za
jamii wanayokabiliana nayo wananchi wa Chalinze ni kielelezo cha wazi cha
kushindwa kwa Rais Jakaya Kikwete, CCM na serikali yake, kuweka mazingira ya
wananchi kujitafutia maendeleo.
Dk. Slaa, alikebehi ahadi zinazotolewa
na CCM na mgombea wake, akisema kuwa amepitia vitabu vya bajeti ya serikali ya
taifa na Wilaya ya Bagamoyo, ambapo amebaini kuwa hazimo kwenye makadirio ya
mapato na matumizi ya serikali kuu na serikali za mitaa.
Alisema ahadi hizo ni ulaghai wa
ahadi ambao wamekuwa wakifanyiwa kwa miaka mingi sasa.
“Nimekuwa nikiambiwa kuwa kwenye
kampeni hizi CCM wametoa ahadi karibu kila kijiji, kila wameahidi kila mahali,
nataka kuwaambia kuwa huu ni mwendelezo wa tabia ya ufisadi inayoendekezwa na
chama hicho, kwa sababu kutoa ahadi za uongo pia ni ufisadi.
“Nimelazimika kufanya utafiti na
kupitia vitabu vyote vya bajeti, serikali kuu na serikali za mitaa, ahadi
wanazotoa CCM kwenye uchaguzi huu wa Chalinze hazimo kwenye bajeti. Hivyo
hazitekelezeki. Hapo ni kitu kimoja kati ya viwili au vyote…ama hawajui kusoma
bajeti au wanataka kufanya ufisadi ili watekeleze,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa pia alitumia fursa hiyo
kujibu madai ya kwamba CHADEMA
kimemtelekeza mgombea wake, kwa viongozi wakuu wa chama hicho kutofika kwenye
kampeni, ambapo alisema kuwa yeye ndiye aliyezindua kampeni kwenye Kijiji cha
Miono akiwa ametokea Kalenga, kisha kampeni zikaongozwa na Makamu Mwenyekiti
Said Issa Mohamed.
DK. Shein afunga CCM
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar),
ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Mohamed Shein, amewataka wakazi wa Jimbo la Chalinze, kutosahau mabadiliko yaliyofanywa na wabunge
wa chama hicho waliowahi kuongoza jimbo hilo na waendelee kuenzi fadhila hizo
kwa kumchagua Ridhiwani Kikwete.
Dk. Shein alitoa ombi hilo wakati
akifunga zoezi la kampeni za chama hicho katika Kata ya Miono wilaya ya
Baganoyo.
Alisema kuwa tangu jimbo hilo
lianzishwe limekua likiongozwa na wabunge wa CCM na kuleta mabadikiko katika
kipindi chote hicho, na hivyo ili kuenzi fadhila hizo wanatakiwa kumchagua
Ridhiwani Kikwete aweze kuwa mbunge katika jimbo hilo.
Aliwaomba kumpa kura mgombea huyo
katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika leo ili aendelee kutekeleza ilani ya
chama hicho kwa yale ambayo hayajakamilika.
Alisema wananchi wanatakiwa kuchagua
CCM ili iendelee kuenzi muungano ambao sasa unaenda kusherehekewa kutimiza
miaka 50.
Alisema wapo watu ambao wanajidai
hawaufahamu muungano huo lakini inatakiwa itambuliwe kuwa upo na kila mmoja analitambua hilo.
Aliongeza kuwa muungano huo upo
katika msingi mkubwa.
Aliwataka wananchi kuheshimu uchaguzi
kwa kufanya kwenda kupiga kura kwa utulivu na amani.
Naye Ridhiwani aliwaomba wananchi
kijitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na wamchague kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Aliwashukuru wananchi wa jimbo hilo
kwa kujitokeza kwa katika mikutano ya kampeni aliyoifanya tangu Machi 14, mwaka
huu.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika
leo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki dunia Januari 22
mwaka huu.
Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Pwani, Ulrich Matei, aliwahakikishia wananchi hali ya usalama na kusema kuwa
ulinzi umeimarishwa.
Matei alisema kuwa katika maeneo
mbalimbali ya jimbo hilo ulinzi umeimarishwa na wananchi wanatakiwa kujitokeza
kwa wingi kushiriki zoezi hilo bila hofu.
No comments:
Post a Comment