`
Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya
Doita, (Chadema), amezitaka halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya watu wenye
ulemavu kupata mahitaji yao badala ya
halmashauri hizo kutenga asilimia 10 kwa ajili ya wanawake na vijana pekee.
Aidha, watoto wenye ulemavu wa
kutosikia, wameiomba jamii kuachana na tabia ya kuwaficha majumbani badala yake
wawapeleke mashuleni kwa ajili ya kupata elimu na kujikomboa kimaisha.
Akizungumza na watoto wenye ulemavu
pamoja na wananchi mbalimbali waliokusanyika kuwasikiliza viwanja vya Soko Kuu jijini Arusha.
Alisema wakati umefika sasa kila kata
kutambua watu wenye ulemavu ili waweze kutengewa bajeti yao na kupata misaada mbalimbali
waweze kuinuka badala ya kuonekana ni mzigo ndani ya familia zao.
Alisema ikiwa halmashauri inatenga
asilimia 10 yaani asilimia 5 inakwenda kwa kinamama na tano inakwenda kwa
vijana huku jamii yenye ulemavu ikiwa haitengewi bajeti .
Naye mwakilishi wa kutetea haki za
watoto pamoja na watoto wenye ulemavu mkoani Arusha, Hafsa Mgaza, aliiomba
jamii kuacha tabia ya kunyanyasa watoto hususan wenye ulemavu kwani kila mtu ni
mlemavu mtarajiwa bali walindwe na kuheshimiwa kama jamii nyingine zenye
mahitaji.
Pia alisisitiza kuwa si jambo jema
kumuona mlemavu akinyanyasika na mwenye viungo akimwangalia.
Aidha, aliiomba serikali pamoja na
taasisi mbalimbali kuhakikisha wanapojenga majengo yanakuwa ni rafiki kwa jamii
hiyo hususan vyooni kwani baadhi yao hupata taabu wanapohitaji kwenda msalani
na maeneo mbalimbali kwa ajili ya mahitaji yao.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa
Arusha, Blandina Mkini, alisema serikali itaendelea kushirikiana na jamii hiyo
katika kuhakikisha haki zao zinalindwa na kutoa rai kwa jamii kuacha tabia ya
kuwabaka watu wenye ulemavu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment