UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
umetishia kuvunja Bunge Maalumu la Katiba iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kitaendelea kutumia rasimu yake badala ya kutumia rasimu ya pili
iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba.
Msimamo huo ulitolewa jana katika
kongamano la wananchi wa Dar es Salaam ambalo lilihutubiwa na makatibu wakuu wa
vyama vya siasa vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF, ambavyo vinaunda UKAWA katika
ukumbi wa Land Mark jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ukumbi huo, Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema UKAWA wapo tayari kususia au kuvunjika
kwa Bunge la Katiba endapo CCM wataendelea kutumia rasimu yao.
Alisema hivi sasa CCM wanafanya hila
za kuhujumu rasimu iliyotolewa na Warioba kwa kutoa rushwa kwa baadhi ya
wajumbe wasikubaliane na mambo mengi yaliyopo kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
Dk. Slaa alisema UKAWA watafikia
hatua ya kuvunja au kususia vikao vya Bunge endapo CCM itakataa kurejesha
dokezo la rasimu halisi ya pili ya Jaji Warioba lenye kifungu 1 hadi 6
kinachojadili masuala ya utawala na muundo wa Muungano.
Alisema UKAWA haitakiwi kuzembea
katika hatua hiyo ya awali, kwa kuwa kifungu 1 hadi 6 ndio msingi mzima wa
Katiba mpya inayotakiwa kupatikana, bila hivyo hakuna katiba.
Dk. Slaa alisema wajumbe hao
wanatumia fursa ya kuingia na rasimu ya CCM ili kuendeleza upotoshaji huo baada ya kufundishwa na Rais
Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge ambapo aliitumia fursa
hiyo kuwapa semina ya kutumia rasimu yao ya CCM.
“Upotoshaji uliofanywa na Rais
Kikwete wakati analihutubia bunge na baadaye kukutana nao ndio unaoendelea
mpaka sasa … UKAWA hawawezi kuvumilia hilo kwa sababu wapo kwa ajili ya
wananchi na si CCM,” alisema Dk. Slaa.
Alisema Rais Kikwete aliitumia nafasi
hiyo vibaya kama Amiri Jeshi Mkuu kwa kulichochea Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) na wananchi kwamba serikali tatu zinaweza kufanya nchi isitawalike,
unaweza kutumia gharama kubwa na hata kama nchi itakopa kwa ajili ya
kuziendesha, itashindwa kulipa.
“Ndugu zangu hizo ni hoja dhaifu
sana, alipaswa azifafanue ni namna gani nchi itashindwa kutawalika wakati
wananchi wenyewe waliyatoa maoni hayo ambayo sasa yanafanyiwa kazi … nia yake
ilikuwa ni kulichochea jeshi na wananchi wayachukue maoni yao,” alisema Dk.
Slaa.
Dk. Slaa alisema Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 ulikuwa wa hiari na si huu wa sasa wa katiba
mpya unaolazimishwa na CCM kwa nguvu na njama nyingu ambazo zote zimegunduliwa.
“Hakuna mwenye nia ya kuvunja
Muungano wetu … hapa kinachotafutwa ni namna gani maridhiano yatafikiwa baina
ya pande mbili kulingana na maoni ya wananchi wenyewe waliyoyatoa katika
mchakato wa awali, ili katiba mpya ya kuongoza vizazi na vizazi ipatikane,”
alisema.
Alitoa mfano wa nchi ya Uingereza
ambayo iliungana kwa hiari na nchi nyingine nyingi za bara hilo kwa zaidi ya
miaka 500, lakini hivi sasa nchi ya Scotland inafanya mchakato wa kujiondoa
katika muungano huo, alidai hivyo ndivyo makubaliano katika suala la Muungano
wa Tanzania unapaswa kuwa.
Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete kutoa
majibu kwa wananchi kuhusu muungano tuliokuwa nao sasa kama ni wa nchi moja
yenye serikali mbili au nchi mbili zenye serikali mbili, ndipo aendelee
kuwachochea watu wake kuhusu serikali mbili anazozitaka.
“Kama mwaka 2010 CCM ilifanya
marekebisho namba 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa kuifanya Zanzibar
iwe nchi kamili, hivyo kuwa nchi mbili zenye serikali mbili … Katiba ya
Muungano ya 1977 pamoja na marekebisho haiyatambui,” alisema.
Alisema kama anataka hivyo, ni vema
akaitisha maoni ya wananchi wa Zanzibar kukubali au kukataa serikali mbili na nchi mbili pamoja na
masharti yatakayowekwa kwa maandishi na sivyo ilivyo sasa.
Alisisitiza kwamba kinachofanywa sasa
na UKAWA ni wananchi na nchi kupata Katiba yao na si ya matakwa ya CCM,
CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vya siasa.
Naye Katibu wa NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe, alimtaka Rais Kikwete kurekebisha hadharani maneno aliyoyatoa katika
hotuba yake ili kuondoa hofu na mkanganyiko kwa wananchii na vikosi vya ulinzi
na usalama kuhusu mchakato wa katiba mpya.
“Hofu na mkanganyiko iliyojengeka ni
lazima ibadilishwe na viongozi wa CCM, hasa Rais Kikwete …ili wananchi
tusiamini kuwa matokeo yoyote ya katiba mpya yana madhara,” alisema Nyambabe.
Nyambabe alisema ili kuziba ombwe la
uongozi wa CCM na serikali, UKAWA ndani na nje ya bunge inatakiwa kuonyesha
dira/njia bora ya kupata katiba mpya kwa amani na utulivu.
“UKAWA nje ya Bunge tunasisitiza
kwamba maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya katiba mpya yaheshimiwe
…tunasisitiza kwamba katiba bora itapatikana kwa maridhiano na si mivutano na
kutunishiana misuli,” alisema.
Naye Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa CUF,
Julius Mtatiro, aliwataka wananchi
wawaamini wajumbe wa UKAWA waliopo katika Bunge Maalumu kuwa wanafanya kazi kwa
masilahi ya nchi.
Mtatiro alisema wajumbe wa CCM
watatumia mbinu na hila kuingiza mambo yao, lakini mwisho wa hayo ni wiki
ijayo, ambapo watafanya uamuzi wa kutoka bungeni.
“Tunawaomba wananchi mfuatilie bunge
wiki ijayo … tusipotimiziwa yale ambayo wananchi wanayataka katika katiba yao
inayozungumzia serikali tatu, jiandaeni kutupokea,” alisema Mtatiro huku
akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment