Aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa
Dar es Salaam. Siku moja baada ya
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini
ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, ‘mzungumzaji huyo ana lake
jambo’.
Sitta akizungumza na gazeti hili juzi
mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22
ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alifafanua kuwa saini ya Nyerere
imeongezwa herufi ‘us’ kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa
kumeandikwa neno ‘Msekwa’ kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema
walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini
walifanya makosa.
Msekwa akizungumza na gazeti hili
jana alisema: “Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi,
lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama
kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo.”
Aliongeza: “Ana lengo gani la kutilia
shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original
ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate
wakati wino upo?”
Maoni mengine
Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Taarifa
kwa Wananchi Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda alisema yote hayo yanatokea ni
kuvuruga hoja iliyopo mezani.
Alisema kitendo cha kupoteza muda
kuzungumzia suala la kuchezewa kwa saini halitakiwi kwani kama maudhui yake
hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe.
“Tusianze kupoteza muda kwa mambo
ambayo hayapo cha msingi wananchi wenyewe waulizwe wanaupenda Muungano au la
lakini tusianze kumtafuta mchawi kuwa saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe
kuhusu Muungano,” alisema Mwakagenda.
Sakata lilivyoanza
Utata huo ulianza wiki hii baada ya
kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya
kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na muundo wake.
Hali hiyo ilitokana na kutopatikana
kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la
Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.
Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2
ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi
kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa
aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati
huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi
Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita
Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo
katika hati hiyo ni ya kwake.
Nahodha alisema kwa maelezo ya
Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya
Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
hali kadhalika.
Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba
uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi
kurejeshwa.
Kwa upande wake Katibu wa Bunge la
Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu,
hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment