Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Jenista Mhagama.
Baraza la Mitihani la Tanzania
(Necta), limejipanga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa sekondari
nchini kwa kusambaza vitabu vya tathimini ya uchambuzi wa ufaulu kwa kila
mtihani uliofanywa.
Usambazaji wa vitabu hivyo
utakafanyika kwa shule zote nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Matokeo
Makubwa sasa (BRN) ili kuwawezesha walimu na wanafunzi kubaini makosa kwenye
mitihani mbalimbali iliyofanywa.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Jenista Mhagama, akizindua vitabu hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, alisema
vitaonyesha tathimini ya ufaulu kwa kila swali katika kila somo, matakwa ya
maswali na jinsi watahiniwa walivyoyajibu kwa kupata au kukosa.
“Uchambuzi huu utawasaidia
walimu na wanafunzi kubaini makosa
mbalimbali yanayofanywa na watahiniwa wakati wa kujibu maswali na hivyo
kujifunza mbinu bora za kujibu maswali hayo, itasaidia kuboresha kiwango cha
ufaulu cha watahiniwa kwa miaka ijayo,” alisema.
Alisema ni vema vitabu hivyo
vikawekwa kwenye tovuti ili wadau wengi waweze kuvisoma kwa njia ya mtandao na
kupata taarifa sahihi ya tathimini ya ubora wa elimu na hivyo kutekeleza
mikakati mbalimbali ya kuboresha kiwango cha elimu.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk.
Charles Msonde, alisema jitihada za pamoja katika kuboresha ufundishaji na
ujifunzaji zinahitajika ili kuongeza ubora wa elimu kwenye masomo yote kwa kuwa
ufaulu kwenye masomo yote uko chini ya asilimia 50.
Alisema chini ya BRN, Wizara
ilijiwekea mikakati tisa ya kutekeleza ambayo ni upangaji wa shule kwa ubora wa
matokeo, utoaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri, kuwa na kiongozi cha
usimamizi wa shule, upimaji wa kitaifa wa stadi za kusoma.
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) (Elimu), Kassim Majaliwa, alisema vitabu hivyo
vitawasaidia walimu na wanafunzi kubainia mambo yenye changamoto katika
ujifunzaji na ufundishaji na sababu za kuwafanya watahiniwa washindwe kujibu
maswali.
Majaliwa aliwaagiza maafisa elimu wa
mikoa, wilaya na kata kufuatilia matumizi ya vitabu hivyo na kuhakikisha kila
shule inapata nakala kwa kuwa ni nyenzo
muhimu katika kufanya kazi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment