bango la kampeni ya kura ya maoni Crimea
Wapigakura katika jimbo la Crimea leo
wanapiga kura ya maoni kuhusiana na iwapo jimbo hilo lijitenge na Ukraine na
kujiunga na Urusi, na kuzusha mzozo ambao ni sawa na uliokuwa wakati wa vita
baridi.
Mzozo huo katika eneo hilo la pembe
ya mashariki mwa bara la Ulaya umeiweka hali ya diplomasia katika mtafaruku.
Kiasi ya watu milioni 1.5 wanapiga
kura katika eneo hilo, ambalo lina idadi kubwa ya watu wenye asili ya Urusi.
Uchaguzi ni kati ya kuwa sehemu ya
Urusi ama kuchukua madaraka zaidi lakini kubakia Ukraine, lakini hakutakuwa na
nafasi ya kuchakua kubakia kama ilivyo hivi sasa.
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa
saa 12 asubuhi na vitafungwa saa kumi na mbili jioni kwa saa za Ulaya ya
mashariki, ambapo matokeo yatapatikana mara baada ya kufungwa vituo vya kupigia
kura, licha ya kuwa kumekuwa na kauli mbiu inayosema "tuko Urusi" ,
mabango hayo yakiwa katika majengo ya serikali, hali ambayo inatoa ishara juu
ya matokeo.
Mataifa ya magharibi
Mataifa ya magharibi yamesema
hayataitambua kura hiyo ya maoni, wakati Urusi ikisisitiza kuwa ni mfano wa
kuamua kujitawala kama ilivyofanya Kosovo.
Majeshi ya Urusi na wanamgambo
wanaounga mkono Urusi wamedhibiti eneo hilo la rasi muda mfupi baada ya rais
anayeungwa mkono na serikali ya Urusi Viktor Yanukovich kuondolewa madarakani
mwezi uliopita baada ya miezi mitatu ya maandamano dhidi ya serikali yake
ambayo yamesababisha umwagikaji wa damu.
Ulinzi mkali kabla ya kura hiyo ya
maoni
Vituo vya kijeshi vya Ukraine katika
eneo hilo, ambalo ni mahali Urusi ilipoweka meli zake za kivita tangu katika
karne ya 18, vimezingirwa lakini hakuna mapambano ya silaha na haijafahamika ni
nini kitatokea kwa vituo baada ya kura hiyo ya maoni.
Waandishi washambuliwa
Kumekuwa na mashambulizi kadha dhidi
ya waandishi habari pamoja na wanaharakati wanaopendelea umoja , mashambulizi
ambayo yameshutumiwa na shirika linalotetea haki za binadamu la Amnesty
International kuwa yanatia wasi wasi mno.
Marekani imepuuzia kura hiyo ikiita
"kura kwa mtutu wa bunduki" na serikali mpya ya Ukraine imeiita kura
hiyo ya maoni kuwa ni batili na ina wasi wasi kuwa Urusi inajaribu kuchochea
uasi mkubwa zaidi katika eneo lenye wakaazi wengi kutoka Urusi upande wa
mashariki ya Ukraine.
Wanaharakati watatu wameuwawa katika
miji wa mashariki ya Donetsk na Kharkiv muda kuelekea kura hii ya maoni kwa
jimbo la Crimea na waungaji mkono wa Urusi wametoa wito wa kuwa na aina hiyo ya
kura katika majimbo mengine ya Ukraine.
Wabunge wa Urusi wameidhinisha rais
Vladimir Putin kuivamia Ukraine wakati akipenda , wakidokeza haja ya kuwalinda
watu wenye asili ya Urusi dhidi ya watu wenye msimamo mkali wa kizalendo.
Ukraine iko katika hali kamili ya
tahadhari kijeshi na katika mkesha wa kura hii ya maoni imeyashutumu majeshi ya
Urusi kwa kukamata kijiji nje kidogo ya Crimea , ikisema, " Ukraine ina
haki ya kutumia hatua zozote zinazowezekana kuzuwia uvamizi wa kijeshi wa
Urusi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Amina Abubakar
Chanzo: DW Swahili
No comments:
Post a Comment