Sunday, November 3, 2013

Waziri: Tofauti ya mfumo wa ushuru wa forodha unaumiza wafanyabiashara



Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Suala la tofauti ya ushuru wa forodha katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, limechukua sura mpya baada ya Serikali kukiri kuwa linaumiza wafanyabiashara.

Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema kuwa tofauti hizo zitaondolewa baada ya sehemu hizo mbili kuanza kutumia mfumo mmoja wa utozaji kodi na ushuru.
Alisema kuwa utaratibu wa kutumia mfumo mmoja wa kulipa kodi unatarajiwa kuanza baada ya makubalino, utapunguza malalamiko ya wafanyabiashara ambao wanadhani hawatendewi haki.

Saada alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia kulipa kodi mara mbili, wanapokwenda Zanzibar kununua bidhaa ambapo pia hulazimika kuzilipia tena wanapofika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakati naibu waziri huyo akieleza hayo, wafanyabiashara wengi wa jijini Dar es Salaam wanalalamika kwamba watu wanaoingiza bidhaa kupitia Bandari ya Zanzibar wanatozwa kiasi kidogo ikiliganishwa na wale wanaoingiza kupitia Tanzania Bara..

Walidai kuwa kontena moja la futi 40 hutozwa kodi Sh2.5 milioni Zanzibar wakati kontena kama hilo hutozwa kati ya Sh25 milioni na Sh30 milioni Tanzania Bara.
Shimbe Kinena ambaye ni mfanyabiashara wa nguo jijini Dar es Salaam alisema kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia Bandari ya Zanzibar hutozwa
ushuru mdogo na baadaye kuingizwa jijini kinyemela kwa njia za panya ikiwamo bandari bubu.

Alisema kuwa hali hiyo inawafanya wanaoingiza bidhaa kutoka nje kupitia bandari na njia za barabara Tanzania Bara kushindwa kuuza bidhaa, zao kwa vile zile zinazoingia kupitia Zanzibar huuzwa kwa bei ya chee.
Waziri Saada akizungumzia madai ya kontena moja la futi 40 kutozwa kodi ya ndogo Zanzibar, ukilinganisha na bara alisema: “Siwezi kuthibitisha kama gharama ndiyo zipo hivyo, ninachojua kwa upande wa Zanzibar malipo yanaweza kuwa hata nusu ya yale ya Bara.”

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema kuwa mfumo mmoja wa ulipaji kodi utaondoa tofauti za viwango vya kulipa kodi vilivyopo sasa.

Hata hivyo, alikanusha kuwa gharama za kulipia kontena moja kwa Zanzibar ni ndogo ikilinganishwa na zile za Tanzania Bara.
“Siyo sahihi kwamba gharama za kulipia kontena Zanzibar ni ndogo sana kuliko Tanzania Bara kwa sababu kinachoangaliwa kwenye kontena ni thamani ya mzigo uliopo ndani na siyo kwamba kuna bei maalumu iliyowekwa,”alisema.

Alisema kwamba kuna viwango maalumu vya kisheria vilivyowekwa kwa pande zote mbili vinavyofuatwa na kwamba vitabadilishwa utaratibu mpya utakapoanza.
Alibainisha kuwa mpango huo unaoratibiwa na Serikali utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa sera husika.

“Hilo ndiyo lengo letu, ni jambo la kisera, ambalo sisi tunaletewa na kutekeleza tu…ubishi uliopo sasa kuhusu tofauti za kodi hautakuwepo,” alisema Kayombo.
Chanzo: Mwananchi

No comments: