Monday, November 11, 2013

Uhaba wa chakula kuikumba mikoa 16



HALMASHAURI 61 katika mikoa 16, zinatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula. Kauli hiyo ilitolewa bungeni juzi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 13 wa Bunge. Alisema halmashauri hizo zipo katika Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora.

Alizitaka halmashauri zinazohusika katika mikoa hiyo, kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye ziada.

Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa chakula hicho kinafika mapema katika maeneo yao kabla wananchi wa maeneo husika hawajaanza kulalamika.

“Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa chakula nchini hadi kufikia Oktoba, 2013 ni ya kuridhisha kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013, ambapo mazao yake yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo mbalimbali nchini.

“Tathimini ya awali iliyofanyika Julai, mwaka huu inaonyesha kuwa uzalishaji wa chakula katika msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013, utafikia tani 14,383,845,” alisema Pinda.

Alisema kutokana na hali ya upatikanaji wa chakula kuwa nzuri, bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika soko nchini zimeendelea kushuka.

Aidha, alisema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), imepanga kununua tani 250,000 za nafaka katika msimu wa mwaka 2013/2014, hadi kufikia Oktoba 23, mwaka huu ulishanunua tani 218,412.

Aidha alizungumzia mpango wa ruzuku za pembejeo, uzalishaji na ununuzi wa mazao ya biashara, operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo mbalimbali, hali ya ulinzi na usalama nchini na utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
chanzo: Mtanzania

No comments: