Sunday, November 3, 2013

Tanzania sasa yashuka kiwango katika kuvutia wawekezaji



Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye anasema ripoti hiyo ya Benki ya Dunia imeshtua taasisi yake na imewasikitisha sana kwa kuwa badala ya kupanda, Tanzania imeporomoka kwa nafasi 11. PICHA | MAKTABA

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kuporomoka kwa nafasi 11 katika kuweka mazingira bora ya biashara na kuvutia wawekezaji kimataifa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Tanzania imeporomoka kutoka nafasi ya 134 mwaka 2013 hadi nafasi ya 145 kati ya nchi 185 katika kuweka mazingira bora ya biashara ili kuvutia uwekezaji ikiwa ya mwisho Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alibainisha hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumzia ripoti ya sasa ya Benki ya Dunia inayotolewa kila mwaka kuhusu mazingira bora ya biashara.

“Ripoti hii imeishitua taasisi yetu na imetusikitisha sana kwa sababu badala ya kupanda, tunashuka na safari hii tumeshuka kwa nafasi 11 hali ambayo siyo nzuri kwa uchumi wa nchi,” alisema.

Benki hiyo inapima hali ya nchi ya ufanyaji biashara kwa kuangalia viashiria vilivyowekwa kimataifa vikiwemo utoaji wa vibali vya ujenzi.
Mkurugenzi huyo wa TPSF ameishauri Serikali kuhakikisha inaongeza kasi ya kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuvutia uwekezaji zaidi.

“Serikali haina budi kuongeza kasi ya kujenga mazingira bora ya biashara ili kuvutia uwekezaji na ina wajibu wa kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara ili nchi isizidi kuporomoka kwenye viashiria vya kimataifa.
Alisema katika kukabiliana hali hiyo watendaji wa Serikali wanatakiwa kufanya kazi kwa vitendo kwani mazingira bora ya biashara ndiyo yanavutia uwekezaji na kukuza pato la taifa.

Ripoti hiyo inataja viashiria vingine vya mazingira bora ya ufanyaji biashara kuwa ni pamoja na upatakanaji wa umeme, kuandikisha rasilimali, upatikanaji mikopo, ulindaji wawekezaji, mifumo ya ulipaji kodi, namna ya kufanya biashara za mipakani, kuingia mikataba, kufungua na kufunga biashara na kuajiri wafanyakazi.
Ripoti inaonyesha viashiria hivyo havijaweza kutekelezwa kwa kasi inayotakiwa na Serikali ili kuhakikisha Tanzania inapanda kutoka pale ilipo.

Imetaja nchi nane bora Kusini mwa Jangwa Sahara zinazofanya vizuri ni pamoja na Mauritius ya 20, Rwanda ya 32, Afrika Kusini ya 41, Botswana ya 56, Ghana ya 67, Zambia ya 83, Morocco ya 87 na Namibia ya 98.

Alisistiza kuwa katika mpango wa kufikia uchumi wa kati mwaka 2025, ni vyema jambo hili likawa katika vipaumbele vya Serikali ili kuzidi kuvutia biashara na uwekazaji.
Alisema Rais Jakaya Kikwete mwaka 2009 aliagiza kazi ifanyike na vikosi kazi viliundwa ili kufikia vigezo hivyo,  lakini kasi haijawa kubwa kutokana na wahusika waliopewa dhamana hiyo kutotimiza vyema wajibu wao.
Chanzo: Mwananchi

No comments: