Friday, November 1, 2013

NAHODHA: HATURUDI NYUMA DRC




Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, jana ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Luteni Rajab Mlima aliyeuawa Oktoba 27 mwaka huu.
Waombolezaji wakiwemo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walionekana kuwa na huzuni kubwa baada ya mwili huo kuwasili katika Uwanja wa Lugalo 521 KJ.

Akizungumza baada ya waombolezaji kutoa heshima za mwisho, Bw. Nahodha alisema Luteni Mlima amekufa wakati akitekeleza jukumu la ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alisema Tanzania haishtushi na mauaji yanayotokea dhidi ya askari wake waliopo nchini humo wakiwa na jukumu zito la kulinda amani hadi hali itakapotulia.
"Tutaendelea kupigania amani ya DRC, vifo vinavyotokea dhidi ya askari wetu haviwezi kuturudisha nyuma," alisema.

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Samweli Ndomba, alisema Luteni Mlima aliuawa akiwa katika eneo la mapambano na vikosi vya waasi wa M23, katika Mlima wa Gavana, karibu na Goma.
Baada ya mwili wa Luteni Mlima kuwasili Lugalo, ndege mbili za kivita zilipita juu ili kutoa heshima ya mwisho. Maziko yake yalifanyika jana jioni makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam

No comments: