Tuesday, November 5, 2013

Mbunge azidi kumbana Balozi Kagasheki bungeni



Dodoma. Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba (CCM), amemshukia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kuwa amebeza kauli ya Bunge na kukejeli chombo hicho kwa kwenda kuzungumzia Operesheni Tokomeza Majangili nje ya Bunge, wakati uamuzi ulishatolewa bungeni.

Mkumba, jana aliomba mwongozo wa Spika kupitia kanuni ya 68 na hatua hiyo aliifanya muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Mbunge huyo alisema juzi wabunge walijadili kwa kina hoja ya dharura kuhusu maonevu wanayofanyiwa wananchi katika Operesheni Tokomeza Majangili.
Alisema hata hivyo Balozi Kagasheki, ameonekana na kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba wabunge wanasema sema tu ndani ya Bunge lakini hawajali rasilimali za taifa.

Alisema waziri huyo pia alisema hatishwi na uamuzi ya wabunge wa kumtaka ajiuzulu na kwamba hatoki hadi aliyemteua abatilishe uamuzi wa uteuzi wake.
“Sasa kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye aliyetoa kauli ya kusitisha operesheni hii ya Tokomeza na kitendo cha kuwakamata Wachina ni zoezi tu la Serikali la kila siku ambalo linaweza kuendelea bila operesheni,” alisema.

Je, mheshimiwa Spika, mheshimiwa waziri aliyetoa kauli ndani ya Bunge na anatoka nje na anabeza kauli ya Bunge, anakejeli Bunge naomba mwongozo wako kama jambo hili linaruhusiwa, “ alisema mbunge huyo.

Spika Makinda aliwaonya wabunge na mawaziri kutotumia vibaya midomo yao.
“Nadhani matumizi mabaya ya mdomo yasitumike kwa sababu tukishakubaliana vitu hapa kwenda kusema vitu vingine ni kuwasha moto pengine uliokuwa unaendelea kuwaka vizuri,”alisema.

Bunge liliazimia kuunda kamati maalumu ya kuchunguza operesheni hiyo ambapo Spika Makinda aliahidi kutangaza wabunge watakaounda kamati hiyo jana.
Akizungumza baada kukamata pembe 706 za ndovu jijini Dar es Salaam, Balozi Kagasheki alisema wabunge wanaomtaka ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete pekee.

Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
Chanzo: Mwananchi

No comments: