Thursday, November 7, 2013

'Mizengwe' katika uvujaji mafuta Nigeria



Kampuni ya Shell inasema ni wahalifu wanaopaswa kulaumiwa kwa uvujaju wa mafuta Nigeria

Shirika la kimataifa la Amnesty International,limetuhumu makampuni makubwa ya mafuta ikiwemo Shell kwa kuficha ukweli kuhusu kuvuja kwa mafuta nchini Nigeria.
Kwa mujibu wa shirika hilo, makampuni ya mafuta hudai kuwa mafuta huvuja kutokana na njama za watu wala sio wako kukosa uadilifu, ili kukwepa kuwalipa fidia waathiriwa.
Amnesty inasema sababu kuu ya uvujaji, huwa mabomba ovyo au kuu kuu ya makampuni hayo ambayo husababisha tatizo hilo.

Ripoti ya Amnesty inasema kuwa mpango wa kufanya usafi baada ya kuvuja mafuta hayo, huwa ina dosari chungu nzima.
Hata hivyo moja ya makampuni yaliyolaumiwa, Shell, imesema kuwa inakana vikali madai yasiyo na msingi.
Ilielezea tatizo la wizi wa mafuta ghafi, ambayo ilisema ndio moja ya vyanzo vya uchafuzi wa mazingira katika eneo la Niger Delta.

Mwandishi wa BBC mjini Lagos anasema kuwa kiwango kikubwa cha mafuta yanayovuja yamesababisha uchafuzi mkubwa sana wa mazingira katika eneo la Niger Delta na uvujaji unafanyika kwa kiwango kikubwa sana .
Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty, kulitokea visa 474 vya uvujaji wa mafuta mnamo mwaka 2012 katika eneo moja pekee, ambalo linamilikiwa na kampuni ya mafuta ya Nigeria Agip Oil.

Ripoti ya Amnesty imetokana na ushirikiano na mashirika ya kijamii nchini Nigeria kufanya uchunguzi kuhusu visa vya kuvuja mafuta kwa kipindi cha miezi sita.
Ripoti hiyo imesema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya makampuni hayo kusema kuwa ni wizi na njama za watu ambazo zimesababisha kuvuja kwa mafuta.
Chanzo: BBCSwahili

No comments: