Sunday, November 3, 2013

Tumeamua kuua elimu yetu



JANA serikali kwa mara nyingine imetangaza matokeo ya darasa la saba na kutoa takwimu zinazoonyesha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao kimeongezeka kikilinganishwa na mwaka jana.

Hata hivyo matokeo hayo yanaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wamefeli somo la Hisabati ambalo mwaka jana lilifanywa kwa staili mpya ya kuchagua majibu, jambo ambalo lililalamikiwa na wadau wa elimu kwamba linashusha kiwango cha elimu nchini.
Tumeyapokea matokeo hayo kwa mtazamo hasi kwa sababu teknolojia iliyotumiwa katika kufanya mtihani inayojulikana kama ‘Optical Mark Reader’, ambayo kila  mtihani maswali yalikuwa ya kuchagua, hatukubaliani nayo.

Mtihani wa darasa la saba ulifanyika Septemba 11 na 12, ambapo watahiniwa walitumia karatasi maalumu za ‘Optical Mark Reader’ na kusahihishwa kwa mfumo wa kompyuta.
Matokeo hayo yametangazwa jana huku Watanzania wakiwa katika hoja ya kupinga utaratibu unaotumika kama vigezo vya ufaulu wa kidato cha nne, ambapo sasa serikali imetangaza vigezo vipya ili kila anayehudhuria darasani awe amefaulu.

Kwa sera hiyo mpya ya elimu, kwa sasa hakuna daraja la sifuri, ila madaraja yameongezewa maksi kuwezesha wanafunzi wengi zaidi wafaulu bila kuzingatia elimu bora inayohitajika kwenye jamii.
Tanzania Daima Jumapili tumeshangazwa na utaratibu wa elimu unaofanywa na serikali.
Kimsingi tukiendelea kufanya siasa katika elimu ni vigumu kuingia katika ushindani wa ajira na nchi nyingine hata za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwenye uhusiano unaolegalega.

Watoto hawa waliotangaziwa matokeo tunaambiwa kiwango cha ufaulu kimeongezeka, lakini Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini, Dk. Charles Mchonde, ameshindwa kujua kama waliofaulu wanajua kusoma na kuandika au la!
Dk. Mchonde amesema kwa suala la kujua idadi ya wanaojua kusoma na kuandika linahitaji muda kulifanyia utafiti.

Sisi tunahoji kauli hiyo ya kiongozi wa serikali, ni muda gani wanahitaji kujua kama waliofaulu wanajua kusoma au la?
Je, ikitokea waliochaguliwa hawajui kusoma na kuandika, nini hatima yao kwenye shule za sekondari ambazo pia huko serikali inatangaza ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tano bila kufeli?

Tumeingia katika kile kilichoitwa matokeo makubwa sasa kwa mbinu mbaya, kuleta matokeo tusiyo na uhakika nayo, huku wanafunzi wanapokwenda sekondari tunawaondolea uwezekano wa kufeli hata kama hawajui ili waonekane tu wamefaulu hata kama hawana elimu bora, je, huku ni kusaidia taifa?

Tunachokiona sisi, ni kuwa serikali imechoka kuzomewa na wananchi kwa kutowajibika kwenye masuala ya elimu. Serikali imeogopa shinikizo la maandamano ya wanafunzi na wazazi kuhusu elimu, badala yake hata matokeo yameanza kutolewa yakiwa na athari za kisiasa.

Kutokana na matokeo yaliyotangazwa na serikali kushindwa kubaini kama waliotangazwa kuwa wamefaulu wanajua kusoma na kuandika, tunasema kuwa watoto hawa hawajafaulu ila wamefaulishwa kwa lengo la kuogopa shinikizo la wananchi ili serikali iseme kuwa sera ya matokeo makubwa sasa inafanya vema.
Sisi tunachelea kuwa tukiendelea kufanya utani katika suala la elimu tutakuwa tunasogeza tatizo badala ya kulikabili na kulitatua.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: