Tuesday, November 5, 2013

BUNGE: MUSWADA WA NHIF KWA WATANZANIA WOTE UHARAKISHWE




Naibu Waziri wa Afya na ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid (HM)
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeitaka Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwasilisha haraka muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa watanzania wote ikijumuisha makundi maalumu ya wazee, watu maskini na walemavu wasio na uwezo ili wanufaike na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bi. Jenista Mhagama wakati akifungua semina ya Bima ya Afya kwa wajumbe wa kamati hiyo mjini Dodoma.
"Sisi kama Kamati tumedhamiria kwamba Watanzania wote wapate huduma za matibabu kupitia utaratibu huu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwani ndio wenye manufaa makubwa kwa wanajamii," alisema.

Akitoa maelezo ya utangulizi katika Semina hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa tayari ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Mfuko kuandaa mapendekezo hayo ili kuhakikisha muswada wa Sheria ya Bima ya Afya unaandaliwa haraka na kuwasilishwa kwa Serikali haraka iwezekanavyo.

Naye Mbunge wa Viti maalumu Bi. Hokololo ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Mfuko kwa hatua na kazi nzuri inayofanya katika kutekeleza majukumu yake. Alisema sasa ni muda muafaka kwa menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuangalia upya suala la uhaba wa dawa kwa kushirikiana na Bohari Kuu ya Dawa.

Akichangia mada, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, ameupongeza Mfuko huo kwa kazi nzuri lakini ametoa angalizo kwamba juhudi zinazofanywa na Mfuko huo hazitakuwa na maana kama Watumishi wa Sekta ya Afya hawatakuwa na utu kwa wagongwa wakati wa kutoa huduma.
Aidha ameishauri serikali kuangalia upya namna ya kuboresha motisha kwa watumishi katika sekta ya afya.

Naibu Waziri wa Afya na ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid kitoa ufafanuzi wa hoja za ujumla za kisera na hasa kuhusu changamoto ya uhaba wa dawa na utendaji wa Bohari Kuu ya Serikali Dawa (MSD) imeiambia Kamati hiyo kwamba kuanzia sasa Dawa zote zitawekwa alama maalumu ya Serikali ili kuwabaini wale wote wanaohujumu juhudi za Serikali na kwa sasa Serikali imekwisha kamilisha mchakato wa kuimarisha Mfumo mzima wa utendaji wa MSD kupitia kwa mkandarasi mshauri aliyepewa kazi hiyo.

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za wabunge, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Hamisi Mdee amesema tatizo kubwa lililopo katika ufanisi wa utekelezaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii katika Halmashauri ni kutegemea uongozi wa Mkoa, Halmshauri na Watendaji.

" Ukiona Mfuko wa Afya ya Jamii unafanya vizuri basi ujue hizo ni juhudi binafsi za viongozi wa ngazi ya Mkoa na Wilaya kama Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa au Wakurugenzi wa Halmashauri na wanapohamishwa tu maeneo hayo kila kitu hurudi nyuma," alisema.

Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo, amesema Mfuko wa Bima ya Afya ambao kwa sasa unasimamia Mfuko wa Afya ya Jamii kwa kutoa ushauri wa Kitaalam unamkakati wa kuongeza wigo wa huduma za CHF ili zipatikane hadi katika ngazi ya hospitali za rufaa ngazi ya Mkoa.

" Hii itawavutia wanajamii walio wengi kujiunga na taratibu hizi za bima maana atakuwa na uhakika wa kupata huduma hadi ngazi ya juu badala ya utaratibu ulivyo sasa'' amesema bwana Mdee.
Chanzo: Mjengwablog

No comments: