Monday, November 4, 2013

CHADEMA YAANZA MIKAKATI 2015




Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, amewataka watendaji wa chama hicho nchi nzima, kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014, Uchaguzi Mkuu 2015.
Bw. Mbowe aliyasema hayo Mjini Kahama, mkoani Shinyanga, mwishoni mwa wiki akiwa katika ziara ya kichama Kanda ya Ziwa Mashariki, inayojumuisha Mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga.

Ziara hiyo imeanza Novemba Mosi mwaka huu, ambapo Bw. Mbowe alikutana na Baraza la Mashauriano la mkoani humo na kukagua uhai wa chama katika kanda hiyo.
Pia Bw. Mbowe alikutana na wadau wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Mashariki na kupanga mikakati ya kuimarisha kanda hiyo.

Novemba 2 mwaka huu, alikutana na Baraza la Mashauriano mkoani Mara na kuwataka viongozi pamoja na wanachama wa Mkoa huo, kuweka mikakati ya kuimarisha hadhi ya chama ili kufanikisha harakati za ukombozi wa nchi na kupigania mabadiliko kama inavyokuwa siku zote.

Ofisa Mwandamizi wa Habari CHADEMA Makao Makuu, Bw. Tumaini Makene, alisema kwa kauli moja, viongozi wa Baraza la Mashauriano Mkoa wa Mara, waliazimia kuanza 'Operesheni Imarisha CHADEMA Mara', ambayo itazinduliwa hivi karibuni na kufanyika Mkoa mzima.

Alisema kupitia uongozi wa kanda wenye mamlaka ya kusimamia na kuimarisha chama katika mikoa yote husika, Bw. Mbowe amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wa kukifanya CHADEMA kiendeleekuwa sauti ya Watanzania wote, wanaosaka haki nchini.

Aliwataka wawe viongozi kwa maneno na vitendo akisisitiza umuhimu wao wa kuwa taswira chanya mbele ya jamii pamoja na kukiwakilisha chama kwa kuzingatia uadilifu, uwezo na uwajibikaji kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania ambao chama hicho kinataka kuwaongoza.

Bw. Mbowe alisisitiza umuhimu wa vikao vya kikatiba, mafunzo na mikutano ya wanachama katika usimamizi, uendeshaji wa chama hasa wakati huu ambao Watanzania wameweka matumaini ya kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kupitia CHADEMA
Chanzo: Majira

No comments: