Monday, November 4, 2013

Wafugaji wataka mifugo yao irejeshwe



WAKATI leo Spika wa Bunge, Anne Makinda akitarajia kutangaza majina ya Kamati Teule ya Bunge ya kushughulikia migogoro ya wafugaji na wakulima, wafugaji wametoa siku 14 kwa Serikali kutaka mifugo yao yote iliyouzwa wakati wa operesheni hiyo, irejeshwe. Suala la migogoro ya wafugaji ni miongoni mwa mjadala mkubwa ulioibuka bungeni wiki iliyopita, ambao umetishia kuwang’oa madarakani baadhi ya mawaziri.

Mawaziri waliowekwa kikaangoni ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. John Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.

Akizungumza mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Ally Lumiye, alisema wamefikia uamuzi wa kutaka mifugo hiyo irejeshwe kwa sababu Serikali ilishatoa agizo la kutaka ng’ombe wote waliokamatwa warudishwe kwa wafugaji, jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.

“Serikali ilitoa tamko, kuwa ng’ombe wote warudishwe kwa wafugaji, agizo hilo lilikaidiwa na watendaji wenye kiburi, sisi kama wafugaji, tunatoa siku 14 kuanzia leo (jana) tunataka ng’ombe wote waliokamatwa warejeshwe kama agizo lilivyoelekeza,” alisema Lumiye.

Alisema kwamba, kama mifugo hiyo haitarejeshwa ndani ya siku hizo, watakwenda mahakamani kudai haki yao kwa kuwa wana ushahidi wa waliohusika na uuzaji wa mifugo yao.

Katika mazungumzo yake, Lumiye aliwataka wafugaji wote nchini kuwa makini na watu ambao watahitaji vielelezo vyovyote zikiwamo risiti za faini walizokuwa wakitozwa wakati wa operesheni hiyo.

Alifafanua kuwa, katika operesheni hiyo, wafugaji walikuwa wanapewa risiti na kusainishwa fomu ya kukiri makosa chini ya Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori ya mwaka 1974 kabla ya kuona faini iliyoandikwa kwenye risiti.

“Wakati huu tunasubiri kamati iundwe, tuna wasiwasi kuwa kuna watu wanaanza kupita kwa wafugaji ili kupoteza ushahidi wa matendo yao.

“Nawaomba wafugaji wote wawe makini wasikubali kutoa risiti kwa mtu yeyote ambaye hajaambatana na viongozi wao,” alisema.

Alisema wakati wa operesheni hiyo, wafugaji hawakuwa na tatizo na operesheni tokomeza iliyokuwa inaendelea, bali wanapinga ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu uliokuwa unafanywa na baadhi ya watendaji.

Alisema kuanzia Januari mwaka 2012 hadi Oktoba mwaka huu, wafugaji tisa wameuawa na zaidi ya 20 wamejeruhiwa.

Pia, alisema ng’ombe 499 walipigwa risasi, 221 walitoswa kwenye maji, 910 walikufa kwa njaa na 889 walipotea katika mazingira tofauti.

“Shilingi 143, 970,000 zilitozwa kama faini na zilizotolewa risiti ni shilingi 8,190,000 na ambazo hazikutolewa risiti ni shilingi 135,780,000.

Naye, Mwenyekiti wa Wafugaji, Kanda ya Magharibi inayoundwa na Mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma na Tabora, Kusundwa Wamarwa, alisema hatua ya wabunge kupigania maslahi ya wafugaji na kufikia kuunda kamati hiyo, imewafurahisha.

Wamshukia Lukuvi

Katika hatua nyingine, wafugaji hao wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, awaombe radhi kwa kuwa aliwaita matapeli.
Chanzo: Mtanzania

No comments: