Monday, November 11, 2013

Zitto: Nimechoka Kuzushiwa na kuchafuliwa



*Afichua siri ya kutishiwa kuuawa
*Asema anajipanga kwenda kortini
*Amwandikia Dk. Slaa kudai kauli ya Chadema

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, ameibuka na kutoa kauli na tamko dhidi ya tuhuma mpya dhidi yake zilizosambazwa katika mitandao ya intaneti katika siku za hivi karibuni.

Zitto, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Mjini, amefanya hivyo akitumia majukwaa mawili tofauti. Mwanasiasa huyo kijana ambaye amejipambanua kuwa mtetezi wa misingi ya utaifa, raslimali za nchi, uchumi na masuala ya utawala bora ndani na nje ya chama chake, alifanya hivyo kwa mara ya kwanza juzi jioni, wakati alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika uwanja wa Kolimba wilayani Kariua, Mkoa wa Tabora.

“Katika umri huu mdogo, nimepigwa mishale mingi ya kisiasa, mimi ni binadamu nina damu, nikipigwa hii mishale damu inatoka, ninaumia, sasa nimechoka kupigwa mishale, lazima sasa tuambiane ukweli,” alisema Zitto.

Saa kadhaa baada ya hotuba yake hiyo, Zitto ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa katika mzozo wa wazi na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya Chadema, alisambaza tamko la maandishi ambalo lilibeba ujumbe unaofanana na ule alioutoa Kariua.

Awali katika mkutano wa Kariua, Zitto alisema alikuwa hayuko tayari kuendelea kukaa kimya pasipo kuchukua hatua zikiwamo za kisheria wakati akichafuliwa.

Alisema alikuwa ameshamwandikia barua Katibu Mkuu wake, Dk. Wilibrod Slaa, akihoji iwapo taarifa ya kumchafua iliyosambazwa katika mitandao ya intaneti chini ya kiichwa cha habari kisemacho “Taarifa ya Siri ya Chadema” ni ya chama hicho au la.

Zitto aliyekuwa akizungumzia matokeo ya ziara yake ya kufuatilia kuhusu fedha zilizofichwa na baadhi ya Watanzania katika mabenki ya Uswisi na kwingineko Ulaya, alieleza kusikitishwa na kile alichodai kuwa ni kikundi cha watu ndani ya Chadema ambacho kimekuwa mstari wa mbele kumpaka matope.

“Wakati nafanya kazi hii ya hatari ya kufuatilia hizo fedha zilizofichwa nje ya nchi, navunjwa nguvu na watu ambao tuko chama kimoja kwani imekuwa ni kawaida unapofanya siasa, lazima upate mashambulizi na sasa nashambuliwa na chama changu.

“Katika hali ya kawaida, wenzagu tulionao katika chama ndio waliopaswa kunipa nguvu, kwani tuna kazi kubwa ya kupambana na ‘lidude likubwa linaloitwa CCM,” alisema Zitto.

Akifafanua na pasipo kutaja jina la mtu, alisema kuna watu wachache ambao hawana kazi ndani ya chama hicho ambao shughuli yao imekuwa ni kugonganisha viongozi ili wagombane.

Akirejea historia ya kuchafuliwa kwake, Zitto alisema hali hiyo ilianza mwaka 2009 baada ya kujitokeza na kugombea uenyekiti wa taifa wa Chadema akichuana na Freeman Mbowe.

Alieleza kushangazwa na hali hiyo ambayo alisema inakinzana na kile kilichotokea mwaka 1995 wakati waasisi wawili wa Chadema, Edwin Mtei na Bob Makani walipojitokeza kusaka uteuzi wa mtu ambaye angekiwasilisha chama hicho katika kugombea urais.

Alisema mara baada ya mmoja wao kupitishwa na chama chao, makundi yote yaliyotokana na harakati hizo yalivunjwa na chama kikaendelea kubakia kimoja.

“Mwaka 2009, niliamua kugombea uenyekiti kwa sababu nilijua katika chama chetu kuna demokrasia inayomruhusu kila mmoja kugombea nafasi anayoona inamfaa. Lakini, kitendo cha mimi kugombea kikaonekana ni nongwa japokuwa wapo wengine waliogombea mwaka 1998 na hakukuwa na migogoro.

“Sasa, watu wanaona uchaguzi (ndani ya Chadema) unakaribia, vurugu na ugomvi vinaanza bila sababu yoyote. Lakini, kwa mtu kama mimi niliyeingia kwenye siasa nikiwa mdogo, najua tumefanya mengi na tumeibua mambo mengi pia,” alisema akijigamba.

Katika taarifa yake ya maandishi aliyoisambaza jana, Zitto aligusia kwa muhtasari kuhusu tuhuma kadha wa kadha ambazo ndizo zilizosababisha aandike barua kwa Dk. Slaa.

“Nilipokuwa katika ziara ya Bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka huu, nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti inayoitwa Taarifa ya siri ya Chadema ambayo pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao ya kijamii.

“Taarifa ya Chadema inasema Chadema kimekuwa kikichunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka CCM ili kuivuruga Chadema.

“Ripoti hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes, ambaye kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola za Marekani 250,000 kupitia kwenye akaunti yake binafsi,” alisema Zitto.

Katika tamko lake hilo, Zitto aliita taarifa hiyo iliyojaa mambo mengi ya kimaadili, kuwa ni ya “kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha”

Mbali ya hilo, Zitto alieleza kusikitishwa, kukasirishwa na kufedheheshwa na taarifa hiyo ambayo alisema ilikuwa ikilenga kumtoa katika nia yake ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao.

Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema hawezi kukubali watu watumie jina lake na uanasiasa wake kumchafua yeye na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.

Zitto katika taarifa yake hiyo alisema tayari raia wa Kijerumani aliyedaiwa kumfichia fedha alikuwa amekana tuhuma hizo kupitia maelezo alyoyatoa kwa viongozi wa Chadema.

Kama hiyo haitoshi, Zitto alieleza kukerwa pia na hatua ya ripoti hiyo kulitaja jina la Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei ikimhusisha na yeye kuficha fedha zinazomhusu yeye.

“Niseme mapema, kwamba tangu kuzaliwa kwangu, sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama,” alieleza mwanasiasa huyo.

Akiendelea, Zitto alisema alikuwa amepokea taarifa za kutishiwa maisha na mtu aliyemtaja kwa jina la Theo Mutahaba ambaye pamoja na mambo mengine alimtaka aache kupambana na masuala ya ufisadi.

“Kwa maana hiyo, natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii, nitahakikisha wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na kuchafuana.

“Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, “Struggle is my life,” alihitimisha Zitto taarifa yake hiyo.
Chanzo: Mtanzania

No comments: