Tuesday, November 12, 2013

PAC: Makinda, Ndugai wanatumika kutuingilia



na Betty Kangonga
MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe, amewataka Spika wa Bunge, Anne Makinda, na naibu wake, Job Ndugai, kuacha kutumiwa na serikali kuingilia kamati za Bunge wakati zikitimiza majukumu yake.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za PAC na ile ya serikali za mitaa (LAAC), Filikunjombe alisema mara nyingi kama kamati wamekuwa wakipokea simu kutoka kwa viongozi hao zinazolalamikia utendaji wao.
Filikunjombe alisema kuwa hatua ya kuruhusu vyombo vya habari kuingia wakati wa kuhoji mashirika na taasisi mbalimbali za umma imesababisha tatizo hadi kufikia viongozi hao kuwapigia simu na kuwataka kutofanya hivyo.

Alisema kuwa hatua hiyo inasababisha kukosa uwajibikaji na uwazi katika masuala ya fedha za umma.
“Tunawaita watendaji waje kujieleza mbele ya kamati juu ya matumizi ya fedha lakini cha kushangaza utaona unapigiwa simu mara na Spika au naibu wake; sasa hii inaondoa dhana nzima ya uwajibikaji,” alisema.

Kwa mujibu wa mbunge huyo wa Ludewa (CCM), taasisi hizo zinapoomba fedha zinafanya hivyo mbele ya umma sasa inashangaza kuhofu kuhojiwa wakati vyombo vya habari vikiwepo.
Alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi hao kuziamini kamati na kuziacha zifanye kazi zake kwa umakini ili kuwa na uwajibikaji.

“Tunaomba pia kuepuka kuzivunja kamati hizi mbili, ni vyema zikaachwa ili zidumu kwa kipindi chote kuliko kuzivunja kwa kuwa zina umuhimu zaidi katika usimamizi wa fedha za umma,” alisema.

Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema kuwa ni muhimu Makinda akaona umuhimu wa kuleta kamati nyingine ili kuwezesha shughuli zilizokuwa zikifanywa na kamati ya POAC zikaweza kuendelezwa.
“Tunafahamu umuhimu wa kamati hiyo, leo tunaona umuhimu wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati zilizovunjwa, hivyo Bunge linapaswa kuzingatia uamuzi unaofanywa,” alisema.

Utouh aliongeza kuwa ni vyema Bunge likaona umuhimu wa kamati hizo ikiwa ni pamoja na kuziwezesha ili zifanye kazi zao kwa umakini.
Naye Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohamed, alisema kuwa kamati hiyo inasikitishwa na kitendo kinachofanywa na ofisi ya Bunge kwa miaka miwili kushindwa kuwapa fedha ili kuweza kukagua miradi ya maendeleo.

Alisema kuwa hivi sasa kamati zimechoka kuwa washauri tu badala yake zimetaka kupewa meno ili ziweze kutembea na askari polisi pindi zinapokwenda kufanya ukaguzi mbalimbali.
“Ili nidhamu irudi katika halmashauri zetu tuna haja ya kupewa meno na kukabidhiwa polisi ili tunapokamata watendaji wabadhirifu tuweze kuwakabidhi kwa vyombo vya dola na wakawekwa ndani ili waogope,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Ndugai alikiri kuwa huko nyuma sheria za Bunge zilikuwa haziruhusu vyombo vya habari kuingia wakati idara mbalimbali zinahojiwa kuhusu matumizi.
Ndugai alisema kuwa kuanzia sasa wanajaribu kuangalia namna ya kuweka uwazi katika suala hilo ili kuviruhusu vyombo vya habari kupata taarifa za matumizi ya fedha za umma.

“Juu ya suala la Utouh, nimelipokea; ninaahidi kulifikisha Bungeni na tutatoa majibu muda si mrefu,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: