Tuesday, November 5, 2013

Chadema wamtimua kikaoni Shibuda

Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (kushoto) akiteta na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafuli walipohudhuria kikao cha Bunge, mjini Dodoma jana, Picha na Edwin Mjwahuzi

Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Shinyanga na Mwanza.Hali ndani ya Chadema inazidi kuwa si shwari kutokana na migogoro inayozidi kupiga kambi. Safari hii ikiwa katika Kanda ya Ziwa Mashariki ambako uongozi mzima wa Mkoa wa Mara, umetimuliwa.

Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, pia amefukuzwa katika kikao baada ya wajumbe kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Hatua hizo zimekuja siku kadhaa baada ya Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kutimuliwa katika kikao cha Baraza la Kanda ya Kaskazini, kwa madai ya kukisaliti chama hicho.

Katika tukio la Kanda ya Ziwa Mashariki, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Mara, Bathlomeo Machage, amevuliwa uongozi na nafasi yake kushikwa na Charles Leyela.
Machage anatuhumiwa kushindwa kuendesha vikao na kuzorotesha maendeleo ya chama kwa jumla.

Ofisa Habari wa Chadema, Tumain Makene, alisema jana kuwa mwenyekiti huyo amesimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali.
Hata hivyo, tuhuma hizo zilipingwa vikali na Machage ambaye alisema hatua hiyo dhidi yake ni batili kwa madai kuwa katiba haivipi mamlaka vikao vya kanda kutimua viongozi.
Alisema yeye bado ni kiongozi halali wa Chadema mkoani Mara.
Alisema uamuzi huo uliofikiwa katika kikao cha viongozi wa Kanda ya Ziwa Mashariki, ulipaswa kufanywa na Baraza Kuu la chama.

Alisema Chadema ni chama cha watu kinachojiendesha kwa misingi ya katiba na kwamba kwa kuzingatia hilo, uamuzi wa kumwondoa katika uongozi unapaswa kufanywa na Baraza Kuu.Alisema mfumo wa uongozi wa kanda ulianza hivi karibuni na kwamba kamwe kikao cha kanda hakiwezi kumfukuza kiongozi wa ngazi ya juu kama yeye.

“Chama kina katiba na kwa mujibu wa katiba hiyo kiongozi wa chama mkoa ni mtu anayechaguliwa na Baraza Kuu, sasa naondolewaje na kikao cha kanda wakati kikao cha baraza hakijakaa, sijaitwa kujieleza wala kusomewa tuhuma zangu,” alieleza Machage.
Alisema tuhuma kwamba ameshindwa kuitisha vikao, hazina msingi kwa sababu jukumu hilo ni la katibu.
Kwa upande wake, Shibuda alisema uamuzi wa kumtoa nje, ulikuja baada ya mjumbe mmoja kutoa hoja ya kumtaka atolewe kwa madai kuwa amekuwa wakihudhuria vikao vya CCM.

Alisema uamuzi huo ulifanyika katika kikao hicho kilichoketi mkoani Shinyanga chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbunge huyo alisema yeye binafsi amesikitishwa mno na hatua hiyo kwa madai kuwa hajawahi kukisaliti chama.

“Mimi siyo msaliti kwa nilichokifanya ni kutetea haki na masilahi ya wapiga kura wangu, wakulima na wafugaji. Pale Meatu nilipanda katika jukwaa la CCM kumweleza katibu mkuu wa chama hicho matatizo ya wapigakura wangu, maana yeye ndiye mwenye serikali iliyoko madarakani hivi sasa,” alisema Shibuda.

Mjumbe aliyetoa hoja dhidi ya mbunge huyo, alikuwa Ahmed Nkunda, kutoka Mwibara.
Kitendo hicho kilisababisha mvutano mkali uliomlazimisha Mbowe kuwatuliza wajumbe na kuamua kuendesha upigaji kura za ndiyo na hapana ili kuona wangapi waliokuwa wakiunga mkono hoja na wale waliokuwa hawaafiki.

Baada ya kuhesabiwa kwa kura za vidole, wajumbe 90 waliunga mkono hoja na wengi 30 waliipinga. Kwa matokeo hayo Shibuda aliamriwa kutoka ndani ya ukumbi wa kikao.
Mwenyekiti wa Chadema katika Kanda ya Ziwa Mashariki, Silvester Nhoja, alisema Shibuda alitolewa kwa matakwa ya wajumbe baada ya mvutano.

“Shibuda alilalamikiwa na wajumbe ambao walimtaka atoke nje , Mbowe alilazimika kuwatuliza wajumbe na kuwataka wampe nafasi Shibuda ajieleze lakini wajumbe waligoma na baadaye zikapigwa kura, zlizoamua Shibuda kutolewa nje,” alisema.
Mvurugano katika chama hicho kinachoongozwa kwa upinzani dhidi ya chama tawala, umekuwa mkali katika siku za hivi karibuni.
Chanzo: Mwananchi

No comments: