Monday, November 4, 2013

DKT. MVUNGI HOI, APIGWA MAPANGA



Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Dkt. Sengondo Mvungi, amejeruhiwa vibaya kwa mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo limetokea nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, saa sita usiku ambapo Dkt. Mvungi alipigwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Akizungumzia tukio hilo, Dkt. Natujwa Mvungi ambaye ni mtoto wa Dkt. Mvungi, alisema watu hao walivamia nyumbani kwa baba yake wakati amelala usiku, kumtaka awape fedha na aliposema hana, walianza kumcharanga mapanga mwilini.
Dkt, Natujwa ambaye pia ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB), alisema baba yake ameumizwa zaidi eneo la kichwani na amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, Bw. James Mbatia, alisema Dkt. Mvungi amelazwa katika Chumba cha Watu Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika hospitali hiyo.

Alisema Dkt. Mvungi ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi UB, baada ya kujeruhiwa na watu hao, alikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha, mkoani Pwani lakini hali yake haikuwa nzuri hivyo alilazimika kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili.
"Tumesikitishwa na tukio hili, baada ya kumvamia na kumjeruhi, watu hao waliiba simu, fedha na kompyuta mpakato (Laptop), wakati watu hao wamevamia Dkt. Mvungi alikuwa amelala, alifikishwa Muhimbili saa 10 alfajiri," alisema Bw. Mbatia.

Aliongeza kuwa, watu hao wamemjeruhi vibaya na hali yake si nzuri sana hivyo madaktari wanaendelea kumhudumia kwa kumpatia matibabu.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura, alikiri kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa, hadi jana jioni msako mkali ulikuwa ukiendelea ili kuhakikisha wahusika
wa tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Ni kweli tukio limetokea kama ulivyosikia...sisi kama Jeshi la Polisi tunaendelea na msako mkali ili kuwakamata wahusika, hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hili," alisema.
Dkt. Mvungi aliwahi kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi
Chanzo: Majira

No comments: