Sunday, November 3, 2013

Wabunge wazuia operesheni ujangili



*Wasema imevunja haki za binadamu, mifugo
*Kamati teule ya Bunge yaundwa kuchunguza

SERIKALI imesitisha ‘Operesheni Tokomeza’ iliyokuwa imeanzishwa kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ujangili katika maeneo mbalimbali nchini. Hatua hiyo imekuja baada ya wabunge kupiga kelele wakipinga operesheni hiyo, wakisema inakiuka haki za binadamu.

Wakizungumza bungeni jana, wabunge mbalimbali walisema operesheni hiyo imeleta matatizo makubwa, ambapo matukio mengi yamefanywa ikiwamo baadhi ya watu na mifugo kuuawa kwa kisingizio cha kusaka majangili. Wabunge hao wamekwenda mbali zaidi na kuitaka Serikali kuwashughulikia watendaji wote waliohusika katika mauaji ya raia na mifugo na wote wachukuliwe hatua.

Serikali kupitia tamko la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, imeridhia hoja za wabunge na kuamua kusitisha operesheni hiyo.

“Wote waliokiuka utaratibu na maagizo ya operesheni, ni lazima hatua stahili zichukuliwe,” alisema Kagasheki.

Baadhi ya wabunge walisimama na kuomba mwongozo wa spika wakitaka Bunge lisitishe shughuli zake na badala yake wabunge wapate fursa kujadili operesheni hiyo ambayo imeleta madhara kwa jamii.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo kuwasilisha taarifa zao ambazo hazikuwaridhisha wabunge.
Said Nkumba
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisema migogoro ya wafugaji na wakulina ni ya muda mrefu, lakini Serikali imekuwa ikishindwa kutatua migogoro hiyo.

“Naomba niweke msimamo wangu, haiwezekani mpaka mambo yanakuwa makubwa kiasi hiki watu wanaathirika, mali zao zinaathirika uhai unapotea ndipo Serikali inakuja hapa kutoa maelezo.

“Kazi ya Serikali ilikuwa kuendelea na hili zoezi walilokuwa nalo, naomba Bunge lichukue nafasi yake ya Bunge liunde kamati itakayofanya kazi ya uchunguzi kwa kina.

“Huko vijijini kuna matatizo makubwa wakulima na wafugaji hawaelewani, kila siku Serikali badala ya kutatua tatizo inaenda kutatua migogoro kwa kutumia mabomu na bunduki, hatuwezi kuendelea na utaratibu wa namna hii.

“Wanaofanya operesheni wanatumia maneno mabaya kwamba wametumwa na Ikulu na uongozi wa juu kwamba hawawezi kuhojiwa, je walitumwa kweli na Rais au Serikali?

“Tunataka tupate taarifa za kina nani wamechukuliwa hatua hadi sasa na majangili wangapi wakubwa wamekamatwa,” alisema Nkumba.
Kangi Lugola
Kwa upande wake, Mbunge wa Mwibara, Alphaxad Kangi Lugola alisema taarifa za mawaziri hao zimetokana na shinikizo la Bunge ambazo zimejaa maneno matamu ya kudanganya Bunge na Watanzania.

“Waziri wa mifugo katika taarifa yako unasema unawapa pole watu kwa usumbufu uliowakuta, hivi kweli jambo hilo limekuwa usumbufu wakati watu wamepoteza maisha?

“Waziri wa Maliasili na Utalii anasema tokomeza ujangili, kumbe ni tokomeza ufugaji na miradi ya watu kujipatia utajiri, mawaziri hawa wataponea wapi kama damu za watu zimepotea.

“Kama Bunge lako litakubali maelezo ya Serikali kwamba ikatathimini hilo haliwezekani, wakati Jeshi la Polisi limeua watu, maaskari wa wanyama pori wameua watu.

“Serikali haiwezi kuwatathimini watu ambao wamewashinda kwa muda mrefu, kazi hii lazima ifanywe na kamati teule ya Bunge lako tukufu,” alisema Lugola.
Dk. Titus Kamani
Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani, aliitupia lawama Serikali na kusema haina tofauti na ugonjwa wa sotoka unaoua mifugo.

Ester Bulaya

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), alisema anashangaa kusikia Serikali inasema imepata mafanikio katika operesheni hiyo kwa kukamata ng’ombe magari na meno ya tembo, badala ya kuwakamata majangili.

“Kama Bunge lazima tufanye kazi yetu, naunga mkono hoja ya kuanzishwa kamati teule, mtandao wa ujangili ni mkubwa, mawaziri wa wizara wanahusika hakuna mkakati wa kupambana na ujangili,” alisema Bulaya.
John Shibuda
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anapaswa kulaumiwa kwa kuwa amekaa kimya wakati taarifa zote za kiintelijensia zinamfikia.

“Wizara ya mifugo ni hasi kwa maslahi ya wafugaji, TAMISEMI ni jiko la dhuluma na jiko la mkakati hasi dhidi ya wafugaji, sheria zilizozaa dhuluma zote zifutwe.

“Tamisemi ipo chini ya Waziri Mkuu, wabunge wa CCM acheni kulalamika, waanze kumuuliza Waziri Mkuu aeleze sababu ya kukaa kimya na kumuachia rais kila kitu akifanye yeye, ningekuwa waziri mkuu ningejiuzulu,” alisema Shubuda.
Kamati Teule
Baada ya Serikali kusitisha operesheni hiyo, Bunge limeunda kamati teule kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya watu na mifugo yaliyofanywa na watumishi wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.

Mbunge wa Kilolo, Peter Msolla (CCM), ndiye alitoa hoja ya kuundwa kwa kamati hiyo, ambayo iliungwa mkono na wabunge mbalimbali waliochangia mjadala huo.

Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR- Mageuzi) alitaka kamati teule inayoundwa na Bunge ichunguze mauaji ya mifugo yaliyofanywa na iende mbali zaidi kwa kuwapima akili waliofanya mauaji hayo.

“Kitendo kilichofanywa na maafisa wa operesheni dhidi ya majangili, walichofanya ni zaidi ya ugaidi, twende mbali zaidi katika kamati kuangalia hata kuwapima akili zao, jambo hili haliwezi kufanywa na mtu mwenye akili timamu,” alisema.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF) alisema mtu anatakiwa alindwe pamoja na mali zake, lakini katika operesheni hiyo watu walinyang’anywa mali zao, wengine walisingiziwa ugaidi.

Alisema hadidu za rejea ziende mbali kuthibitisha ugaidi wao, kwani hilo litasaidia kuona haki inatendeka.

Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM), alisema katika hadidu za rejea yaongezwe majukumu katika kamati ikiwemo kutafuta ni kwanini operesheni hiyo badala ya kutafuta majangili wakauawa mifugo na wafugaji.

“Lazima tukubali hoja ya kuunda kamati ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, mifugo imepigwa risasi imekufa na mashamba yameteketea,” alisema.
Hadidu za rejea
Spika wa Bunge, Anne Makinda alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Ardhi, Profesa Peter Msolla kuhitimisha hoja yake aliyotoa.

Msolla alilitaka Bunge kuunda kamati hiyo ambayo pamoja na mambo mengine itashughulikia migogoro ya wafugaji na wakulima.

Msola alizitaja hadidu za rejea sita. Hadidu hizo ni pamoja na kuangalia na kuchambua masuala ya ardhi na kuangalia mikakati mbalimbali ya Serikali na kuchunguza utekelezaji wake.

Nyingine ni kuchambua mikakati na kusuluhisha migogoro kati ya wafugaji na wakulima, kuangalia mikakati ya kulinda vyanzo vya maji na uhatibifu mazingira na kutoa mapendekezo na kuangalia mambo mengine yoyote ambayo kamati itaona inafaa.

Baada ya Msolla kuhitimisha hoja hiyo aliwaruhusu wabunge kuziboresha hadidu hizo, ambapo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alitaka kabla ya kamati hiyo kuanza kazi ipitie taarifa za tume na kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa kuchunguza masuala ya ardhi.

Mnyika pia alitaka Kamati hiyo iangalie suala la uwajibikaji kwa viongozi wote watakaobainika walifanya uzembe wa kiutendaji katika suala hilo.

Kwa upande wake, Spika Makinda alisema majina ya wajumbe watakaounda kamati hiyo yatatangazwa Jumatatu.
Chanzo: Mtanzania

No comments: