Tuesday, November 5, 2013

‘Msitegemee ajira serikalini’



                                                    na Edna Bondo
WATANZANIA wametakiwa kuacha mazoea ya kutegemea ajira serikalini, badala yake wawe wabunifu kwa kujiajiri.

Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam jana na Mawakala wa M-Pesa Dar es Salaam na Morogoro walipokuwa wakikabidhiwa fedha taslimu na vyeti kutoka Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao.
“Vijana wengi wamekuwa na fikra tegemezi, wamekuwa watu wa kusubiri serikali iwapatie ajira huku wakijua kabisa kuwa fursa za ajira katika ofisi za serikali au sekta binafsi ni chache kuliko nafasi za kujiajiri,” alisema Ziadi Kamanya anayefanya kazi zake Buguruni sokoni.

Juma Nyange, mkazi wa Tabata alisema Watanzania wamekosa ubunifu na ni wachoyo wa kutumia maarifa waliyonayo katika kujiendeleza na kuwaendeleza wengine.
Amina Issa, mkazi wa Tumbaku-Morogoro alisema: “Nilitamani kuwa mjasiriamali wa aina nyingine mara baada ya biashara ya kuendesha pikipiki kunishinda, niliwafuata watu wengi ili wanieleze manufaa yanayopatikana katika biashara hii ya M-Pesa.

“Wengi hawakuniambia ukweli lakini sikukata tamaa baaada ya kujua ukweli na kupata mafanikio ninajisikia furaha sana kwani sasa maisha yangu yanaenda bila wasiwasi.”
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano  Vodacom, Joseline Kamuhanda,  alisema wataendelea kuthamini na kutambua mchango wa mawakala wao wote nchini kwa kuboresha maisha yao.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: