Sunday, November 17, 2013

BLOGU ZA TZ ZAGEUZWA VITUO VYA KURUSHA PICHA ZA UCHI NA NGONO?



MAKALA TIME NA CHIWAMBO
Ni siku nyingine tena wasomaji wangu wa safu hii ya Makala Time na Chiwambo nazungumuzia “Athari za Blogu na Magazeti ya Udaku hapa Tanzania”. Katika ulimwengu wa sasa hasa katika kipindi hiki cha mapinduzi ya vyombo vya habari kutoka mfumo wa zamani wa urushaji matangazo yaani “Analogia”  na kuingia mfumo mpya wa urushaji matangazo kwa vyombo vya habari yaani “Digital” mabadiliko hayaepukiki katika tasnia ya vyombo vya habari nchini.

Kutokana na hilo, Tanzania tumeshuhudia mapinduzi haya ya vyombo vya habari na kutamba kwa Blogu na Wavuti tofauti tofauti ambazo zilizo nyingi huondeshwa bila kuzilipia. Mapindizi haya ya vyombo vya habari yameleta mfumuko wa fikra tofauti tofauti katika uandishi wa makala na taarifa ndani ya  blogu zetu. 

Utafiti  uliofanywa na Mlipa Media Group inayomiliki Chiwambo’s Blog inaonyesha wazi kwamba zaidi ya asilimia 60% ya blogu zinazorusha habari hapa Tanzania ni blogu za Udaku zinazojihushisha na urushaji wa picha za ngono, Habari za mapenzi, pamoja na urushaji wa habari ambazo hazina ukweli. Pamefikia mahari hata wasanii wanapoandaa video zao picha hurushwa wakimaanisha kitu tofauti na uhalisia.

Malalamiko kama haya yamethibitishwa siku ya alhamisi pale msanii wa Bongo (Jina Limehifadhiwa) alipojitokeza mbele ya chombo cha habari cha Clouds FM kipindi kinachorushwa na Mirrard Ayo, kupinga madai ya Blogu hizo kwamba picha hizo zimepigwa wakiwa wanafanya mapenzi kumbe ilikuwa ni maandalizi ya video yake mpya aliyomshirikisha mchezaji wa mpira maarufu hapa Tanzania.

Athari za Blogu na Wavuti kwa wanajamii
Blogu kwa sasa zimekuwa ni kama vituo vya kurushia habari za Ngono, Video za ngono, Habari za Uchonganishi na za uzandiki. Pamefikia mahari hata zile Wavuti na Blogu zilizotegemewa hapa Tanzania kwa kurusha habari za ukweli na uhakika nazo zimegeuka na kurusha habari za udaku ikiwemo picha za nusu uchi au zinazoonyesha sehemu za siri za wanawake.

Wanaoathiriwa zaidi na picha hizi ni wanawake pamoja na wanafunzi. Pamefikia mahari mtu maarufu asimamapo na mwanamke au mwanaume anapigwa picha na kurushwa mtandaoni. Swali la kujiuliza, tunaelekea wapi wanahabari wenzangu? Haya ni madhara ya mtu kujua kusoma na kuandika na kujipachika kuwa yeye ni mwandishi wa habari. Yaani mtu akiweza kuandika barua naye hujiita ni mwanahabari. 

Matokeo yake ndio haya yanayoonekana leo. Blogu kama zingetumika ipasavyo kwa kuwahabarisha Watanzania wenzetu habari muhimu tungeweza kuendelea. Zipo habari nyingi za kurusha hapa Tanzania hasa huko vijijini. Magazeti, Wavuti na Blogu zetu zimeshindwa kuwafikia Watanzania waliopo vijijini ambao hushindia mihogo na uji au mlo mmoja kwa siku. Huduma zimekosekana, miundombinu kama barabara nazo ni aibu upu. Maisha ya Mtanzania leo ni ajabu, wanaishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Kwanini habari kama hizi zisirushwe ili serikali ione nini inachowafanyia wananchi wao. Ijapokuwa kuna Uhuru wa kutoa na kupokea habari, hatuna budi vyombo vyetu kuwa vyombo vya habari vya watanzania “The voice of the voiceless”.  Badala yake tumevigeuza vyombo hivi na kuwa vituo vya kuandika habari za ngono. 

Kama leo hii ningeulizwa swali moja tu na mtu yeyote kuhusu nini kinachokukera ningesema “Vyombo vya Habari vya Udaku hasa Blogu” na ningependekeza vifungiwe ili kulinda utu wa watu wetu. Hivi jiulize swali moja tu. Je ungependa watoto na wajukuu wako wazione picha zako za ngono? Huko  ndiko tunakoelekea kwa sasa. 

Athari za blogu hizi ni kwamba, tunawafundisha watoto wetu  kuingia katika ngono na biashara ya ngono wakiwa na umri mdogo sana. Hivi kama wewe ni mwandishi wa blogu, utajisikiaje pale utapoikuta picha ya mtoto wako imetupiwa pale ndani ya blogu yako au nyinginezo? 

Wanafunzi na picha za ngono mtandaoni
Wanafunzi wetu kuanzia sekondari hadi vyuo vikuu imekuwa ni fasheni kwa baadhi yao kupiga picha za uchi na ngono na kuwapa wanablogu au kuzivujisha mtandaoni. Wasomi wa leo na wa jana ni tofauti kabisa. Wasomi wa jana waliheshimu sana utu wao na tamaduni za kitanzania lakini wa leo hawajiheshimu baadhi yao hasa wasomi wetu wa kike. Hivi baba yako akibahatika kuiona picha yako ukiwa uchi au unafanya ngono atajisikiaje au wewe utajionaje?  Hao ndio wasomi wetu wa leo. Somo la maadili limekuwa kikwazo kwao. Tunatengeneza taifa la weusi lenye giza mbele yake. 

Nini  kifanyike kuzuia uvunjifu wa sheria
Swala kubwa ni wanablogu wenyewe kujiheshimu kwanza. Kuthamini watu wengine na kujithamini wenyewe. Wanablogu wawe wakwanza katika kupinga urushaji wa picha za ngono zinazozidi kusambaa mtandaoni siku hadi siku. Mwanablogu pekee ndiye anayeweza kuzuia blogu yake isiweke picha za ngono ili kuweza kuzuia wimbi la watoto wadogo kutembelea kwenye picha kama hizo. 

Kitu cha ajabu ni kwamba baadhi ya hao wanaorusha na kuongoza blogu hawajui sheria za kujilinda pale watapokubwa na kesi juu ya wanachokiandika yaani “Law of Defamation and its element. 

Haya yote ni madhara ya mfumo wetu wa elimu na inaonyesha namna gani watanzania hawajakombolewa na elimu. Bado tupo ugenini katika elimu. Tunafanya elimu yetu kama kitu kisicho na umuhimu. Tunapeleka wapi elimu yetu? Tunatengeneza “Taifa la Vilaza, Mambumbumbu, na Majuha” na hao ndio viongozi wetu hapo baadaye sisi tutapoaga na kuondoka.
Imeandikwa na Ausi Chiwambo

Phone No. 0753110740

No comments: