Monday, November 11, 2013

Makubaliano ya amani kutiwa saini leo Jumatatu?




Rais wa DRC Joseph Kabila, (kulia),Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala.
Waasi wa kundi la M23 na serikali ya Kongo wanatarajiwa kutia saini makualiano ya amani tarehe 11.11.2013 mjini Kampala wiki moja baada ya M23 kutangaza kusalimu amri vitani

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la maziwa makuu Mary Robinson amesema kwamba makubaliano ya amani yanayosubiri kutiwa saini kesho Jumatatu na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kundi la waasi la M23 ni hatuwa muhimu kwa ajili ya amani katika kanda hiyo.

Halikadhalika mjumbe huyo ameapa kwamba jeshi la taifa na kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa chenye mamlaka ya kuingilia kati vita hivyo vitaendelea kwa pamoja kushirikiana katika juhudi za kuyamaliza makundi mengine ya waasi mashariki ya Kongo.
''Kuna mitazamo tofauti juu ya kinachofanywa na serikali na Monusco kwa pamoja mashariki ya Kongo lakini sasa makundi yote ya waasi yatashughulikiwa'' amesema mjumbe huyo ambaye ni rais wa zamani wa Ireland.

Kundi la waasi la M23,mojawapo ya makundi yenye silaha yanayoendesha operesheni zao katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini lakini masikini kabisa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo limepata pigo kubwa na hatimae kusalimu amri baada ya kukabiliwa na jeshi la taifa likiungwa mkono na kikosi maalum cha Monusco.Kundi hilo la M23 linatarajiwa kutia saini makubaliano ya amani mjini Kampala nchini Uganda Jumatatu mkataba ambao unaiweka katika mchakato rasmi ahadi yao ya kuachana na uasi wa miazi 18 pamoja na kulivunja kundi hilo.

Pongezi kwa Jeshi
Bibi Robinson amelipongeza jeshi la Kongo akisema ni jambo la kutia moyo kuona jeshi la Kongo FARDC likipata ushindi dhidi ya kundi la waasi na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu kama jeshi la taifa.Halikadhalika mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema ni kitu kizuri kwamba mchakato wa Kampala unafikia mwisho wake kwa kutiwa saini kwasababu kuna maelewano juu ya kuwajumuisha wapiganaji wa M23 katika jeshi la taifa au alau kuwaruhusu kurejea nyumbani.Ama kwa upande mwingine ameyataja mafanikio hayo pamoja na kutiwa saini makubaliano ya Kampala siku ya Jumatatu ni hatua zitakazofikisha mwisho madhila na mateso ya muda mrefu kwa raia wa jimbo la Kivu.

Kipaombele
''Umekuwa muda mrefu wa mateso yasiokubalika na sasa kuna matumaini ya kweli'' amesema bibi Robinson.Kitakachopewa kipaombele nchini Kongo kwa mujibu wa bibi Robinson ni mapambano sasa dhidi ya waasi Wakihutu kutoka Rwanda waliokita kambi nchini Kongo FDLR,kundi ambalo ni sehemu ya wapiganaji wa Kihutu wenye msimamo mkali waliohusika katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda.


Serikali ya Rwanda inayoongozwa na kabila la Watutsi walio wachache inalitazama kundi hilo la FDLR kama kitisho kikubwa cha usalama kwa taifa lake na imekuwa ikituhumiwa na Umoja wa Mataifa kuhusika katika kuwaunga mkono waasi wa M23.Mary Robinson amezungumzia suala hilo akitowa kauli ya kutaka kishughulikiwe kiini cha kuzuka makundi haya.

''Nadhani imetambulika kwamba kuna haja ya kushughulikia sababu za ndani,kwa kuwa kiini cha kuibuka kundi la waasi la M23 ni kilio cha kweli cha Watutsi ambao hawajihisi kuwa nyumbani ndani ya nchi yao wenyewe na hapa tunazungumzia Kongo''
Mwandishi:Saumu Mwasimba/Afp

Mhariri:Mohammed Dahman
Mjumbe  wa  ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasema raia wa Congo wanafuraha juu ya uwezekano wa kupatikana amani kufuatia ripoti kuwa serikali ya Kinshasa itatia saini makubaliano na waasi wa M23 hii leo Jumatatu.

Bebe M’poko balozi wa DRC huko Afrika Kusini anasema serikali ya DRC inapanga kudhibiti zaidi usalama kwenye mipaka yake ili kuwalinda raia wasio na silaha kutokana na mashambulizi ya makundi mengine yenye silaha. Alisema mzozo wa taifa hilo unachangiwa pia na wale ambao wanataka kuizuia DRC kunufaika na raslimali zake kubwa.

Bw M’poko anasema vita hivyo vinaendelea  kwa sababu kuna watu ambao wanataka kupora raslimali za Congo na kuiweka Congo katika hali isiyo thabiti.

Anasema raslimali hizo zingewanufaisha watu wa Congo, bara la Afrika na hata ulimwengu mzima, kwa sababu Congo ni eneo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini, mafuta, utalii na kadhalika.

Anasema jeshi la congo litaweza kulinda mipaka ya nchi hiyo ambayo imekuwa wazi na hivyo kuwezesha makundi yenye silaha kuingia kutoka nchi jirani.

Wote DRC na kundi la waasi wa M23 wanatarajiwa kutia saini makubaliano ya amani hii leo, katika mji mkuu wa Kampala, Uganda. Hatua hiyo inafuatia miezi ya majadaliano baina ya pande hizo mbili na tangazo la kundi la M23 kuwa linaweka chini silaha zao, baada ya vikosi vya jeshi la DRC kuwan’goa kutoka ngome zao zilosalia wiki jana.
Chanzo: DWSwahili & VOASwahili




No comments: