Tuesday, January 21, 2014

JK atema wengine watano, wapya ni 10

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akitangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Picha na Edwin Mjwahuzi

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo yamewatupa nje mawaziri watano, kuwaingiza 10 wapya, kuwapandisha manaibu wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wengine wanane kutoka wizara zao kwenda nyingine.

Miongoni mwa walioachwa katika mabadiliko yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa ambaye nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge.

Wengine walioachwa na wizara zao kwenye mabano ni Manaibu Waziri, Goodlucky Ole Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Gregory Teu (Viwanda na Biashara), Benedict Ole Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).

Mawaziri hao wanaungana na waliokuwa mawaziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais kutokana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Balozi Sefue alisema kuachwa kwa mawaziri hao ni moja ya hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete kuimarisha utendaji serikalini. Pia alisema mabadiliko hayo yametokana na kuwapo kwa nafasi baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.

“Rais amefanya mabadiliko kwa mujibu wa Ibara ya 55 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka ya kutekeleza wajibu huo,” alisema Balozi Sefue.

Sura mpya

Sura 10 mpya zilizoingia katika Baraza hilo ni pamoja na Dk Asha Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani ambaye anakuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Naibu wake, Kaika Saning’o ole Telele ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro.

Wengine wapya ni wale walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri na wizara zao kwenye mabano, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (Fedha), Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).

Pia wapo Mbunge wa Serengeti, Dk Steven Kwebwe (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi (Kilimo, Chakula na Ushirika), Mbunge wa Mufindi Kusini, Mahmoud Ngimwa (Maliasili na Utalii) na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).

Waliopandishwa, kuhamishwa

Mbali na Dk Mahenge, Rais Kikwete pia amewapandisha manaibu waziri wengine watatu kuwa mawaziri kamili pasipo kuwahamisha wizara walizokuwa. Hao ni Saada Nkuya Salum anayekuwa Waziri wa Fedha, Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii).

Balozi Sefue alisema Rais Kikwete amewahamisha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuchukua nafasi ya Dk Nchimbi, wakati aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi amerejeshwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kuchukua nafasi ya Nahodha. Dk Mwinyi aliwahi kuongoza wizara hiyo.

Wengine waliohamishwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuchukua nafasi ya Charles Kitwanga aliyehamishiwa Wizara ya Nishati na Madini kuendelea na wadhifa huo. Kitwanga anachukua nafasi ya George Simbachawene ambaye amehamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima amehamishiwa Wizara ya Fedha kuchukua nafasi ya Janeth Mbene ambaye amehamishiwa, Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua nafasi ya Teu. Amos Makalla amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwenda Wizara ya Maji.


Sefue alisema mawaziri na manaibu waziri wapya wataapishwa leo saa 10 jioni Ikulu.
Chanzo: Mwananchi