Rais Kikwete akipitia hotuba atakayoisoma katika Bunge Maalum la Katiba alipokuwa katika ndege kuelekea mjini Dodoma jana.
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), limemtahadharisha Rais Jakaya Kikwete asiingie kwenye mtego
wa wanasiasa wa chama chake cha CCM wanaoiponda Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa bungeni Jumatatu kwa kuwa ndiyo iliyobeba maoni ya wananchi.
Wasiwasi wa Jukata umekuja baada ya
baadhi ya viongozi wa Serikali na makada wa CCM, anachokiongoza kutoa kauli za
kuipinga Rasimu hiyo hadharani.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Makamu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema Rais Kikwete kesho
(leo), atalihutubia Bunge Maalumu la Katiba na akiikashifu Rasimu hiyo atakuwa
amejikashifu mwenyewe kwa sababu tume hiyo ipo kisheria.
“Mambo yaliyomo kwenye Rasimu hiyo si
ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe
wenzake, bali ni maoni ya wananchi hivyo yanatakiwa kuheshimiwa,” alisema.
Mwakagenda alisema kazi iliyofanywa
na Tume hiyo iheshimiwe na wabunge waendelee kuiboresha kabla haijapigiwa kura
ya maoni na wananchi.
Akizungumzia kuchaguliwa kwa
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na Makamu Mwenyekiti Samia Sululu Hassan, Mwakagenda alisema
utendaji wao wa kazi unahitaji kufuatiliwa kwa karibu kwa sababu wote ni
mawaziri wa Serikali na makada wa CCM.
“Licha ya viongozi hawa kusifika kwa
uadilifu, kwa nafasi zao za uwaziri kuongoza Bunge Maalumu la Katiba kunawaweka
katika mtego wa kuingiliwa katika utendaji wao,” alisema na kuongeza:
“Jukata kwa niaba ya Watanzania
inaahidi kuwafuatilia viongozi hawa wakati wote wa kuongoza Bunge Maalumu la
Katiba kwa kuwashauri, kuwaonya na kuwarekebisha watakapokosea.”
Kuhusu tabia ya kuzomeana,
alisema kitendo hicho kinalivuruga Bunge
na kusababisha wabunge kuacha kujadili masuala waliyotumwa na wananchi.

No comments:
Post a Comment