Tuesday, March 25, 2014

MICHEZO: Mashine mpya sita Msimbazi

KOCHA Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic ametamka mambo mawili. La kwanza inawezekana lisiwe zuri sana kwa mashabiki wa Msimbazi lakini la pili ni la maana.

Kwanza amewaambia mashabiki wasiwe na matumaini makubwa kutokana na  hali halisi ya ufanisi wao wa uwanjani lakini pili, amewahakikishia kwamba atashusha Msimbazi mashine sita mpya za maana ambazo zitabadili kila kitu na kurejesha heshima ya klabu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu, Logarusic alisema Simba inahitaji nyota wapya wenye uwezo na uzoefu mkubwa wasiopungua sita ambao ndiyo watakaoweza kuleta matokeo mazuri wakichanganywa na baadhi waliopo sasa lakini akasisitiza kwamba atafanya mabadiliko makubwa ambayo yatarejesha heshima ya Simba msimu ujao.

Alisema atasajili mabeki wawili wa maana, viungo wawili viwango pamoja na mashine nyingine mbili za kufunga magoli.  Alisema Simba inahitaji viungo wawili wenye uwezo wa kuchezesha timu ikiwa ni pamoja na kutoa pasi za mwisho kwa washambuliaji ambazo sasa ni wazi zimepungua.

“Kwasasa ni kama kila kitu kimemalizika msimu huu, huu ni wakati wa kuanza kujipanga kwa msimu ujao, tunatakiwa kufanya marekebisho makubwa kwa kuleta nyota wapya wasiopungua sita ambao watachanganywa na baadhi ya waliopo sasa,” alisema Logarusic ambaye Simba bado haijampa mkataba mpya kwani ule wa awali unamalizika mwisho wa msimu huu.

“Hawa waliopo sasa sio kwamba wote hawafai, wapo wanaofaa kwa kubakia katika timu hii, wapo wengine wanaotakiwa kukaa benchi kujifunza kutoka kwa wengine au kuwarudisha nyuma kidogo katika kundi la vijana na pia wapo ambao wanatakiwa kuondolewa kabisa,”alisisitiza.

Tayari Simba imeshaanza mikakati hiyo ya kuboresha kikosi ambapo Mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Pope alimuagiza  mkurugenzi wao wa ufundi, Moses Basena kwenda nchini Uganda kuangalia nyota wapya wanaowataka.

Basena alisharudi nchini kurudisha ripoti ya awali ambapo katika ripoti yake hiyo inasemekana amekuja na mikataba ya nyota hao ambao wamemvutia kulingana na vigezo alivyopewa na Logarusic akisubiri kumkabidhi Hanspope ambaye yupo safarini kikazi.

Simba imepoteza matumaini ya ubingwa ambapo sasa inasaka nafasi ya pili ingawa bado inakumbana na ugumu wa Mbeya City ambayo imekomaa kwenye nafasi ya tatu ikaziba njia ya Simba kupenya.

Chanzo: Mwanaspoti

No comments: