Thursday, March 27, 2014

BUNGE LA KATIBA: VIWANGO VYA SITTA VYAPATA MSUKOSUKO

FALSAFA ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ya kuongoza Bunge hilo kwa kasi na viwango, jana iliingia doa; na kulazimika kuahirisha Bunge hilo baada ya kiti chake kutuhumiwa kuyumba katika kutetea kununi zilizopitishwa na Bunge hilo wiki tatu zilizopita.

Hali hiyo ilijitokeza bungeni mjini Dodoma jana muda mfupi baada ya Bunge hilo kuanza, ambapo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alianza kuchangia kwa kutuhumu kiti cha Mwenyekiti wa Bunge hilo kutetereka na kushindwa kusimamia kanuni.

Alisema ndani ya Bunge hilo viporo vya kanuni vilivyokuwa vimebaki bila kutolewa maamuzi vilihusu kanuni ya 37 na 38 zinazohusu utaratibu wa upigaji kura, lakini inashangaza kuona wamepewa jedwali lingine lenye mabadiliko ya kanuni kinyume cha utaratibu.

"Mheshimiwa Mwenyekiti hapa tumeletewa jedwali lenye marekebisho ya kanuni maalumu ambazo tayari zilipitishwa na Bunge Maalumu na kuridhiwa," alisema Lissu.
Alitaja kanuni ambazo tayari zilikuwa zimeridhiwa na Bunge hilo, lakini zilipelekwa zikiwa kwenye jedwali hilo kwa ajili ya kufanyiwa mabadiliko kuwa ni kanuni ya 14 (1), 32, 33,35 na 51 (1) D.

Alitaja kanuni nyingine kuwa ni 63 (1), 64 (1) ambayo ilipitishwa na azimio la Bunge na ile ya 85 (4). Lissu alisema mabadiliko hayo ya kanuni yamesainiwa na Katibu wa Kamati ya Uongozi ya Bunge badala ya mwenyekiti.
Alisema kuwasilishwa kwa jedwali hilo la mabadiliko ya kanuni ni kinyume cha kanuni ya 87 (2) ambayo inaeleza utaratibu na mapendekezo ya marekebisho ya kanuni.

"Sasa kanuni hazina hata wiki tatu mnaanza kuzichakachua... hiki mnachotaka kukiingiza hapa kisiingizwe mpaka yatakapoletwa mapendekezo ya kanuni ya 37 na 38," alisema Lissu na kuongeza kuwa; "Kamati ya uongozi haina mamlaka na mambo ya kanuni."
Lissu alienda mbali zaidi na kusisitiza kuwa; "Hii ni takataka isiingizwe ndani ya Bunge hili, huu ni ubatili." Akikazia zaidi msimamo wake, Lissu alisisitiza; "Hatuwezi kuruhusu uchafu wa namna hii, hii ni takataka."

Lissu wakati akitoa hoja zake alikuwa akishangiliwa na baadhi ya wabunge na wengine kuzomea. Baada ya Lissu kumaliza kuwasilisha hoja hiyo ya kupinga jedwali hilo la marekebisho ya kanuni, ndipo alipofuata zamu ya Mwenyekiti wa Bunge, Sitta ambapo alisema; "Hizi ni tuhuma nzito kwa mwenyekiti wa Bunge (Sitta) na zinaelekezwa kwake wakati hicho kinachoongelewa hajakiona." Alisema maelekezo yalitoka kwa Kamati ya Uongozi kwenda kwenye Kamati ya Kanuni ni halali.

Sitta, alielezea kushangazwa kabisa na hali iliyokuwa inatokea bungeni. Wakati hali ya mvutano ikiendelea, huku kukiwa na hali ya kutoelewana na wabunge wengine kuzungumza bila kupewa nafasi na kiti, Sitta alikuwa alitumia busara kuwatuliza wabunge hao bila ya mafanikio.

Baadaye Sitta, alitoa nafasi kwa Mwanasheria wa Serikali y a Mapinduzi Zanzibar, Abubakari Hamis, ambaye alianza akishangazwa na msingi wa kutaka kufanyika kwa mabadiliko hayo ya kanuni katika Bunge hilo.

Alisema kifungu cha 87 (2) cha kanuni walizozipitisha kinaeleza utaratibu wa kubadili kanuni, hivyo mtu hawezi kujifunga na kufanya mabadiliko bila kufuata utaratibu. "Hatukubali kanuni kubadilishwa badilishwa kinyemela, chochote ambacho kitaenda kinyume cha taratibu hatutakubali, fuata kanuni, ukishafuata kanuni tutaheshimu lakini kinyume hatutakubali," alisema.

Baada ya hapo Sitta, alimpa nafasi Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, Jaji Frederick Werema, ambaye kabla ya kuanza kutoa hoja zake alikumbana na zomeazomea kiasi cha yeye kukiri kuwa hajazoea kuzomewa. Alisema analoliona yeye ni kuwahisha hoja bila kusoma kanuni vizuri na kuzielewa. Alisema kanuni ya 87 fasihi ya kwanza inaeleza vizuri jinsi ya kuzifanyia marekebisho kanuni hizo.

Mbunge wa Bunge hilo, Ismail Jussa Ladhu, alisema inashangaza kuona kanuni ambazo hazijaanza kutumika kasoro zake zinaanza kuonekana. "Kasoro yake yameonekana wapi?" Alihoji?

Baada ya kumaliza kusikiliza hoja za wabunge, Sitta alisema migogoro ya kanuni huamuliwa na Kamati ya Kanuni za Bunge. Alisema yote yaliyosemwa yawe mazuri au mabaya anayapeleka kwenye kamati ya kanuni za Bunge yawe mazuri au mabaya.
Hatimaye mwenyekiti aliahirisha Bunge hadi leo jioni.

Chanzo: Majira

No comments: