Tuesday, March 25, 2014

MICHEZO: Yanga yaipigisha Azam mchakamchaka

AZAM ina basi kali la kifahari, uwanja wa maana na wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi nchini na wanaoishi kitajiri zaidi lakini mastaa wake wametamka kwamba wana mchakamchaka wa hatari ndani ya siku 18 kukata ngebe za Yanga.

Matajiri wametamka kwamba wana safari ya siku 18 ambayo inaanza kesho Jumatano nje ya uwanja wao wa nyumbani kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara, wanaamini kwamba wakishinda vita hiyo na kurejea Dar es Salaam salama basi wana uhakika wa asilimia zote kuwa mabingwa wapya wa soka nchini.

Azam imesaliwa na mechi tano tu kumaliza ligi msimu huu lakini kati ya hizo mechi nne itacheza kwenye viwanja vya ugenini wakati Yanga inayowakimbiza kwenye mbio za ubingwa ikiwa imesaliwa na mechi mbili tu ugenini kati ya sita ilizonazo kumaliza msimu.

Safari hiyo ya siku 18 nje ya uwanja wao wa Azam Complex  itacheza mechi nne mfululizo kabla ya kurejea uwanjani hapo Aprili 19 kucheza mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.

Matajiri hao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 47 kibindoni kesho watacheza na Mgambo JKT mjini Tanga ikiwa ni mechi yake ya kwanza katika safari hiyo. Baada ya hapo itarejea Dar es Salam kucheza na Simba kabla ya kurejea tena mikoani.

Azam inayosaka ubingwa Bara kwa mara ya kwanza tangu iasisiwe mwaka 2007 itasafiri tena kwenda kucheza na Ruvu Shooting mkoani Pwani Aprili 6 kabla ya kupaa kwenda Mbeya kucheza na Mbeya City Aprili 13.

Safari hiyo itahitimishwa kwenye mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu Aprili 19 kwenye uwanja wa Azam Complex.

Kocha msaidizi wa Azam, Ibrahim Shikanda alisema kuwa licha ya timu yao kuwa na mechi nyingi ugenini bado wana imani ya kufanya vizuri kwani timu yao imekua na historia nzuri katika mechi ilizocheza ugenini kwa msimu huu.

Kiungo wa timu hiyo Salum Abubakar ‘Sure boy’ alisema, “Mechi za ugenini huwa zinakuwa ngumu lakini kwa kuwa tumedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu ni lazima tujitahidi kushinda mechi zote hizo.”

Naye mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche alisema: “Timu zinakamia sana kwa sasa hususani zilizoko kwenye hatari ya kushuka daraja lakini kwa kuwa timu yetu ni kubwa na inahitaji ubingwa ni lazima tupambane kuonyesha kuwa sisi ni bora.”

Azam itacheza mechi zake za ugenini ikiwa na rekodi nzuri kwani katika mechi tisa ilizocheza ugenini imefungwa mabao manne pekee ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja katika viwanja hivyo vya ugenini.

Mshambuliaji wao, John Bocco alisema: “Kazi kubwa tunayo wachezaji katika kipindi hiki kigumu ambacho ligi inaelekea ukingoni kwa kila timu kupambana ili ichukue ubingwa na nyingine zisishuke daraja, hivyo lazima tushinde mechi hizi zilizobaki tuchukue ubingwa.”
Chanzo: Mwanaspoti



No comments: