Saturday, March 29, 2014

Wananchi kuvunja Bunge

           Picha ya Maktaba ikionyesha siku ya Ufunguzi wa Bunge maalumu la Katiba hapa Tanzania
JUKATA yaandaa maandamano kushinikiza livunjwe
MWENENDO usioridhisha wa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma umesababisha wanaharakati, taasisi, vyama vya siasa na watu wa kada mbalimbali kutamani Bunge hilo livunjwe.

Moja ya taasisi zilizoamua kuvalia njuga suala la kuvunja Bunge hilo ni Jukwaa la Katiba (JUKATA), ambalo limejitoza kuwaongoza wananchi wenye uchungu na taifa lao na walio nje ya Bunge kujitokeza na kuungana katika harakati za kutaka kulivunja Bunge hilo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Jukata imepanga kuandaa maandamano makubwa ya wananchi kutoka jijini Dar es Salaam hadi Dodoma, kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete alivunje Bunge hilo kwa madai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimevuruga mchakato wa kupatikana Katiba Mpya.

JUKATA imesema kuwa imeamua kufanya hivyo kwa kile ilichodai kutoridhishwa na mwenendo na kasi ya Bunge hilo ambalo tangu Rais Kikwete alipolizindua rasmi, limepoteza mwelekeo kwa kuibua malumbano na makundi ya kiitikadi yanayopigania masilahi binafsi, huku CCM ikionyesha dhahiri kutaka kupata Katiba yenye masilahi kwa chama hicho tawala.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa JUKATA, Hebron Mwakagenda, alisema kuwa Jukata itatumia Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania kuwaongoza wananchi katika harakati hizo.

Ibara hiyo inaelekeza kuhusu mamlaka ya wananchi, ikiwemo wananchi ndio msingi wa mamlaka ya nchi na serikali inawajibika kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa maandamano hayo ya kihistoria, yataanzia jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma na kuwataka wananchi wenye uchungu na upotevu wa fedha zinazotumika kwa wajumbe wa Bunge hilo Dodoma, wajitokeze kuhakikisha Bunge hilo linavunjwa na kutafuta utaratibu bora zaidi wa kuandika Katiba Mpya.

Mwakagenda alisema kuwa wamefikia hatua hiyo kwani hawaridhishwi na namna Bunge hilo linavyoendelea kwani halionyeshi kama linaweza kuwapatia Watanzania Katiba Mpya.

Aidha, alisema kuwa tangu Rais Kikwete alipolihutibia Bunge na kumshambulia Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, utulivu umezidi kukosekana na imeathiri mwelekeo wa Bunge hilo na kuzidisha mgawanyiko.

Alimlalamikia Rais Kikwete kwa kupingana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoichagua yeye mwenyewe, ambayo awali alikuwa akiisifia kwamba imefanya kazi nzuri.

“Rais alipewa nafasi ya kuhutubia  Bunge, matokeo yake akainanga hotuba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni sawa sawa na kujipinga yeye mwenyewe na kuwapinga Watanzania waliotoa maoni yao,” alisema.

Mwakagenda alisema hotuba ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa,  haikupaswa kutolewa na mkuu huyo wa nchi ambaye kazi yake ni kuliunganisha taifa na kuhubiri amani, upendo na maridhiano, hasa katika kipindi hiki cha kupata Katiba mpya.

Katika hatua nyingine, Jukata imebaini kuwa tangu kuanza kwa Bunge la Katiba viongozi wa serikali wamekuwa wakiwatisha waandishi wa habari kwa kisingizo cha kuwa wazalendo.

“Wao wanawatisha wanahabari kwa misingi ya kuwa wazalendo na waandike kile ambacho serikali inataka, tunataka serikali iache vitisho kwa wanahabari ili waweze kufikisha habari kwa wananchi, ili wakati wa kupiga kura ya maoni, waweze kufanya maamuzi yatokanayo na habari walizopewa,” alisema.

Aidha, alisema wanalitaka Bunge hilo kusitisha kutumia kura kama njia ya kufikia maamuzi ya kupitisha katiba, na kuwataka waige utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kikao chao cha kupitisha kanuni kilivyofanya kazi.

“Uzoefu duniani unaonyesha kuwa kinachoongoza utengenezaji wa katiba ni hoja, ushawishi, mijadala, muafaka na maridhiano na si kupiga kura na kuzomeana na kutukanana, upigaji kura ukiendelea madai ya Katiba mpya yataendelea hata baada ya kupitisha katiba hiyo,” alisema.

Alisema kuwa Katiba inayotengenezwa ni ya Watanzania wote na si ya wanasiasa na viongozi, hivyo kitendo cha wanasiasa na viongozi kuwa na sauti kubwa katika utengenezaji wa Katiba kumefanya mchakato huo utekwe na wao ambao idadi yao ni asilimia 85.

Mwakagenda alisema kitendo cha kutumika misimamo ya chama chochote cha siasa katika kutengeneza katiba ni kosa na kimesababisha mabishano kuwa ya vyama vya siasa na Bunge hilo kugawanyika kiitikadi na kimisimamo, hasa katika suala la Muungano.

Kelele za kutaka Bunge hilo livunjwe zimekuwa zikitolewa na watu wa kada mbalimbali, wakiwemo baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo.

Juzi mjumbe wa Bunge hilo, Lekule Leizer, alipendekeza kwa Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge, Samuel Sitta, kuandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete ili alivunje kama muafaka wa aina gani ya kura itumike kwenye maamuzi hautapatikana.

“Kamati ya kanuni imefanya kazi hii kwa shinikizo la kuridhisha pande zote mbili, sasa kama tutaendelea kubishana hapa bila kupata muafaka tunaomba Rais avunje Bunge turudi nyumbani,” alisema.

Laizer alisema inatia uchungu kuona wajumbe wakiendeleza mivutano huku wakilipwa posho wakati hakuna kazi yoyote wanayoifanya zaidi ya kubishana na kuzomeana.

Naye Freeman Mbowe, alishauri suala hilo lirudi kwenye Kamati ya Maridhiano ili viongozi waridhiane badala ya kuendelea kupoteza muda kwa kulumbana kwa jambo ambalo hawataweza kufika mwisho.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: