Tuesday, March 25, 2014

MICHEZO: TAIFA STARS MPYA WAANZA KUJIFUA TUKUYU

WACHEZAJI 29 kati ya 34, waliochaguliwa katika programu maalumu ya marekebisho ya timu ya Taifa, inayoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wameshaanza mazoezi ya nguvu wilayani Tukuyu, Mbeya.

Wachezaji hao, ambao wametokea katika mikoa mbalimbali nchini, waliingia kambini Jumamosi wakiongozwa na kocha Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwagata, ambaye ni kocha wa makipa, Meja Joakim Mashanga daktari wa timu na Fred Chimela Meneja Vifaa.

Taifa stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa mwaka wa pili mfululizo sasa, inatarajiwa kupata mabadiliko makubwa ndani ya miezi miwili ijayo ili ipatikane timu bora itakayoshiriki mechi za kufuzu kucheza Kombe la Afrika.
Makocha wazoefu walikusanyika Lushoto takriban wiki mbili zilizopita na kufanya zoezi la kuwachagua vijana 34, ambao baadaye watachujwa na kubali 20.

Watakaochaguliwa watajiunga na Taifa Stars ya siku zote na kutengeneza timu ya wachezaji 45 ambao watachujwa tena, ili ipatikane timu ya wachezaji 25.
Kazi hiyo inatarajiwa pamoja na mambo mengine kuimarisha uzalendo miongoni mwa wachezaji watakaochaguliwa na hili linafanyika kwa kuhakikisha wachezaji wote, wanaimba wimbo wa taifa kila asubuhi na jioni kabla ya kuanza mazoezi.

Kila chumba cha wachezaji pia kina bendera ya taifa, taratibu za kambi na wimbo wa Tanzania Tanzania ambavyo vinasaidia kuimarisha uzalendo miongoni mwa wachezaji.
Kwa upande wake kocha, Mayanga alisema vijana wote wako salama na wanategemea kuwapata wachezaji wazuri, baada ya kambi hiyo.

ìTunawapongeza wadhamini wetu Kilimanjaro Premium Lager, ambao wamefanikisha shughuli hii kwani tuna imani tutapata vipaji vikubwa mno baada ya zoezi hili na timu yetu ya taifa itakuwa bora zaidi,î alisema.

Timu hiyo imepiga kambi katika hoteli ya Landmark, mjini Tukuyu na wanafanya mazoezi katika Chuo Cha Ualimu.

Shughuli hiyo imeleta msisimko mkubwa mjini Tukuyu, huku mashabiki wa soka wakisema wana imani sasa itapatikana timu bora zaidi kwa sababu ya utaratibu uliotumika.

No comments: