Sunday, March 23, 2014

Sera mbovu kiini kuporomoka elimu


Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wameichambua elimu ya Tanzania na kueleza kuwa, tatizo la kuporomoka kwa elimu ni matokeo ya sera na mifumo mibovu na si uhaba wa miundombinu kama madawati, vitabu au majengo.

Pia wamesema, Serikali inatakiwa kulitangaza tatizo la matokeo mabovu ya mitihani ya wanafunzi kama janga laTaifa, ili liweze kutiliwa mkazo kwa lengo la kushughulikiwa ipasavyo.

Hayo yalisemwa jana katika kongamano la kujadili mchango wa tafiti huru katika kuboresha elimu ya Tanzania, lililoandaliwa na Taasisi ya Uwezo Tanzania lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akitoa mada iliyosema, “ Kwa nini jitihada zetu za kuboresha elimu hazizai matunda”, Mkuu wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Twaweza, Rakesh Rajani alisema kinachotakiwa kuboreshwa ni sera za elimu , ili kuendana na matakwa ya elimu inayotakiwa kufundishwa kwa wananfunzi.

“Hapa tatizo siyo uhaba wa walimu, madawati na majengo’ Tatizo lipo katika mfumo na sera zake, hata tukiboresha yote hayo bila kuzingatia sera hakuna tutakachovuna,” alisema Rajani


Aliongeza: “Miaka minane imepita kila mwaka bajeti ya Wizara ya Elimu inaongezwa, lakini matokeo bado ni mabovu, tunatakiwa kujiuliza wapi tunakosea na kuhoji fedha hizo zinakwenda wapi kama zinaongezwa na hakuna tofauti.”

Naye Mratibu wa Taasisi ya Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla alisema “Matatizo ya elimu nchini yatangazwe kama janga laTaifa, tukiendelea kuwapeleka hivyo hivyo tutegemee kupata wataalamu walio chini ya uwezo.”

Mgalla alisema, Serikali inajivunia ongezeko la watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza, lakini swali la kujiuliza je, wanakwenda shule wanajifunza?

Kwa upande wake, Profesa Mstaafu Justinian Galabawa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Elimu, alisema serikali inatakiwa kutenga vipaumbele vichache vya Taifa, ambavyo itaweza kuvisimamia na kuvitekeleza.

“Tukiwa na vipaumbele vingi hatutaweza kuvisimamia, tuisimamie elimu walimu, wanafunzi majengo na rasilimali zote zinazohusu elimu hata kama ni kidogo zisimamiwe ipasavyo,” alisema Profesa Galabawa.
Chanzo: Mwananchi



No comments: