Tuesday, March 25, 2014

Nyalandu amtimua kigogo mwingine Utalii

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amemfukuza kazi Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB), Dk. Aloyce Nzuki, kwa madai ya kutokuwa na imani naye katika utendaji kazi wake.

Akitangaza hatua hiyo jana mbele ya waandishi wa habari, Waziri Nyalandu alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo, wajumbe wa Bodi ya Utalii walimwandikia barua ya kutokuwa na imani na Nzuki.

Waziri huyo ambaye tangu awe waziri kamili kuongoza wizara hiyo amekuwa katika harakati za kusafisha watendaji wabovu na wabadhirifu, alisema ameamua kuchukua hatua hiyo haraka ili kunusuru sekta ya utalii nchini ambayo imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu.

“Baada ya kuletewa barua ya malalamiko hayo, nilijipa muda kufanya uchunguzi na kujiridhisha kwamba mkurugenzi huyo ana matatizo, ndipo nikachukua uamuzi huo,” alisema Nyalandu.

Waziri Nyalandu ameagiza kutangazwa mara moja kwa nafasi hiyo, ambapo Mtanzania yeyote mwenye sifa bila kujali yupo ndani au nje ya nchi, anaruhusiwa kutuma maombi ndani ya siku 21, kuanzia leo.

Aidha, alisema uteuzi wa mkurugenzi  huyo utafanywa na taasisi zenye utaalamu katika masuala ya utalii ambapo watatakiwa kupendekeza majina tisa kabla ya yeye kuyafikisha kwa Rais Jaka Kikwete kwa hatua zaidi za uteuzi.

Wakati mchakato wa kumpata mkurugezi mpya ukiendelea, Waziri Nyalandu alisema katika kipindi kilichobaki, Mkurugenzi wa Masoko, Devota Mdachi, atakaimu nafasi hiyo.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Charles Sanga, alisema kabla ya uamuzi huo, tayari wajumbe walikuwa wameridhia kujiuzulu nafasi zao kutokana na mkurugenzi huyo kwa muda mrefu kuyumbisha kazi za kitalii.

Hata hivyo pamoja na matamko hayo, Waziri Nyalandu alikataa kuulizwa swali lolote na waandishi wa habari ambao walibaki eneo hilo wakiwa na maswali mengi, ikiwemo kama ana mamlaka ya kufanya hivyo, ukizingatia kwamba  mwenye mamlaka ya uteuzi huo ni rais.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: