Wednesday, March 26, 2014

Pakistan kuzungumza na Taliban

                                                             Wapiganaji wa Taliban
Kundi la waakilishi wa serikali nchini Pakistan linasafiri kuelekea katika eneo la wapiganaji wa Taliban Kaskazini Magharibi mwa taifa hilo.
Kundi hilo linaelekea huko ili kufanya mashauriano ya amani na kundi la wapiganaji wa kiislamu nchini Pakistan.
Hii ni mara ya kwanza kwa waakilishi wa serikali kufanya mkutano wa moja kwa moja na kundi la wapiganaji wa Tehreek-i-Taliban.

Mazungumzo hayo ni harakati za waziri mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif, kutafuta mbinu ya kukomesha ghasia ambazo zimesababisha vifo vya watu wengi.
Wajumbe hao wa serikali waliondoka mapema leo kuelekea katika eneo lisilojulikana Kaskazini magharibi mwa pakistan ili kukutana na wanachama wa baraza la kisiasa la Taliban.

Ajenda ya mkutano huo hata hivyo haijawekwa wazi,lakini inadaiwa kushirikisha makubaliano ya kuongeza mda wa kusitisha vita ambayo yanatarajiwa kukamilika wiki ijayo mbali na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa.

Askari jeshi katika eneo lililoshambuliwa na Taleban nchini Pakistan
Kundi la taliban linataka watu linaowataja kuwa 'wasiopigana' kama vile wanawake na watoto waachiliwe.

Lakini serikali imekana kumzuia mwanamke yeyote ama mtoto katika jela zake.
Wachanaguzi wanasema kuwa serikali nayo itataka kundi hilo kuwaachilia waathiriwa wa utekaji nyara akiwemo mwana wa aliyekuwa waziri mkuu.

Mwezi uliopita ,baraza hilo la wapiganaji wa taliban lilitoa matakwa yake ikiwemo kuwekwa kwa sheria ya kiislamu nchini humo,serikali ya Pakistan kuwaondoa wanajeshi wake katika maeneo ya vijiji mbali na serikali hiyo kuvunja uhusiano wake na Marekani.
Katika majuma matatu ambayo makubaliano hayo ya kusitisha vita yaliafikiwa,kumekuwa na mashambulizi mabaya katika mji wa Islamabad na Peshawar,hata hivyo kundi la Tailban limekana kutekeleza mashambulizi hayo.

Chanzo: BBC Swahili

No comments: