Sunday, March 30, 2014

RAIS KIKWETE: Mali za serikali zirasimishwe

RAIS Jakaya Kikwete ameagiza mali zote za serikali zikiwemo nyumba, zirasimishwe kwenye miliki ya serikali kwa kutafutiwa, kupatiwa hati na nyaraka muhimu.

Taarifa iliyotolewa juzi jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema, Rais Kikwete alitoa agizo hilo ili kuweka rekodi sahihi ya mali za serikali.

Alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, aliyekwenda Ikulu kuwasilisha Ripoti ya Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka jana.

Rais Kikwete aliagiza kazi hiyo ianze mara moja na ikamilike haraka kwakuwa utaratibu huo utasaidia kuzuia baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kupora na kuchukua mali hizo, zikiwamo nyumba.

Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na Utouh, kuhusu changamoto mbalimbali walizokumbana nazo wataalamu wa Ofisi ya CAG katika kufanya ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na miradi mbalimbali.


Alibainisha kuwa historia inaonyesha kuwa, tangu enzi za ukoloni, mali za serikali hazina hati wala nyaraka rasmi za kuthibitisha umiliki wa serikali, hali iliyotoa mwanya kwa watu wasio waaminifu kuvamia, kudai na hata kuzipora.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: