Wednesday, March 26, 2014

Afungwa miaka 70 kwa kulawiti

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi  imemhukumu kifungo cha miaka 70, Forensi  Albeto (34) baada ya kupatikana na hatia  ya kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka 10.

Hukumu hiyo ilitolewa  jana na Hakimu  Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa, ambapo alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa.

Mshitakiwa  alidaiwa kutenda kosa hilo  hapo Novemba  mwaka jana akiwa nyumbani kwake  alipokuwa akiishi  na mama mzazi wa mtoto huyo Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Godfrey Ruzabila, alidai kuwa mshitakiwa alikuwa akimlawiti na kumbaka mtoto huyo nyakati za usiku .

Ilidaiwa  mtoto huyo alikuwa akiishi  na bibi yake  na alikuwa akienda kuishi na mshtakiwa mama yake alipokuwa anaugua ili awe akimsaidia kazi.

Ruzabila, alidai kuwa mshtakiwa na mkewe walikuwa wakiishi kwenye nyumba yenye chumba kimoja huku mtoto huyo alikuwa  akilala sebuleni.

Mshitakiwa alidaiwa kuwa alikuwa akitoka chumbani kwake nyakati za usiku  kutekeleza unyama wake wa kumbaka na kumlawiti mtoto huyo.

Inadaiwa mshtakiwa alikuwa akimtishia kumuua mtoto huyo endapo atapiga kelele au kusema kwa watu anavyotendewa.

Ruzabila alidai mahakamani kuwa baada ya mtoto huyo  kuona  baba yake anaendelea kumfanyia unyama huo aliamua kutoroka nyumbani na kuelekea mjini Mpanda kwa lengo la kumtafuta dada yake  amueleze anavyofanyiwa.

Mwendesha Mashitaka aliieleza mahakama baada ya mtoto huyo kumtafuta  dada yake bila mafanikio aliamua kwenda Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mpanda ambapo polisi walimchukua hadi  Hospitali ya Wilaya ya Mpanda na kufanyiwa vipimo.

Alidai taarifa ya daktari ilionyesha kuwa mtoto huyo amelawitiwa   na kubakwa na aligundulika akiwa ameambukizwa magonjwa ya zinaa.

Akitoa hukumu, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga Ntengwa, alisema baada ya kusikiliza ushahidi na utetezi mahakama imemtia hatiani mshtakiwa.

Ntengwa, alisema mahakama  imemwona na hatia ya kifungu  cha sheria  namba 130, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili na 131,154 cha kanuni ya adhabu.

Hakimu huyo alitoa fursa kwa mshtakiwa Foresi Albeto, kujitetea ambapo aliiomba mahakama imwachie huru kwa kile alichodai kuwa  ushahidi uliotolewa na mtoto wake huyo wa kambo  alifundishwa na polisi.

Hakimu Chiganga Ntengwa  alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa na inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 70 jela kwa kubaka na kulawiti.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: