Na Abdallah Khamis, Igunga
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
analipwa sh milioni 384 kwa mwaka, sawa na sh milioni 32 kwa mwezi pasipo
kukatwa kodi.
Hii ni mara ya pili kwa Zitto
kutangaza hadharani mishahara ya viongozi wakuu wa serikali, akiwa ameanza na
ule wa Waziri Mkuu, aliyesema analipwa takribani sh milioni 26 kwa mwezi.
Akiwahutubia wananchi mjini Igunga
jana, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama Kanda ya Magharibi,
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema kuwa sababu ya kutaka
mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ijulikane, ni kuzuia mianya ya watu
wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo hilo.
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi
wanacholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi, bali ni usiri unaofanywa
juu ya kiwango hicho jambo alilosema kuwa linaweza kutumiwa na wajanja
kuendelea kuinyonya nchi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona
mwalimu anayelipwa mshahara wa sh 220,000 kwa mwezi akikatwa kodi, huku
viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi
licha ya kuhudumiwa kila kitu na serikali.
Aliongeza kuwa katiba ya sasa Ibara
ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara pamoja na malipo mengine, huku
ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupurupu kupunguzwa,
hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa
manufaa ya nchi.
"Kwa hiyo hata kesho kama Dk. Willibrod Slaa akiwa rais na akataka kupunguza
mshahara wake, kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa
ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka serikalini," alisema Zitto.
Akiwa katika Kata ya Choma, Zitto
alikagua kilichokuwa kiwanda cha kuchambulia pamba cha Giner ambacho kimeacha
kufanya kazi tangu mwaka 1998.
Alisema kufa kwa viwanda vingi vya
uzalishaji nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Rais mstaafu wa
awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, akidai kuwa alishindwa kutofautisha suala la
uwekezaji na biashara huru.
"Ni serikali ya Mkapa ndiyo
ilitufikisha hapa katika kupotea kwa viwanda nchini, wao walidhani biashara
huru ni kuwapa wawekezaji viwanda vyetu na serikali kujiweka pembeni, sasa nchi
imebaki kutegemea uchumi wa uchuuzi badala ya uzalishaji," alisema.
Alisema sera ya uwekezaji katika
Serikali ya CCM ilichukuliwa kama fursa ya viongozi wa chama hicho kujinufaisha
na mali
za serikali pasipo kujua wataendeleza vipi.
Zitto alisisitiza kuwa kila mara
CHADEMA imekuwa ikisisitiza bungeni juu ya kupiga marufuku usafirishaji wa
pamba kwenda nje kama malighafi, na badala
yake wakitaka viwanda vifufuliwe kwa ajili ya kutoa ajira kwa Watanzania.
Alirejea kusisitiza sera ya hifadhi
ya jamii kwa wakulima akisema imefikia wakati serikali kupitia SSRA ione
umuhimu na ulazima wa kuhakikisha wanaongeza Watanzania wenye hifadhi ya jamii
kwa kuanza mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa wakulima (Supplementary scheme
for social security to small holder farmers).
"Ninapendekeza serikali ichangie
nusu kwa nusu na mkulima ili kuvutia uwekaji akiba katika nchi na kuwa na sera
ya uwekezaji katika maeneo yatakayomwinua mkulima kama miundombinu ya
umwagiliaji, mikopo nafuu kwa wakulima kwenye pembejeo na nyumba na bima ya
afya.
"Nimezungumzia umuhimu wa uwazi
katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi wa
umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega kuwa siku ya Jumanne kamati yangu ya Hesebu
za Serikali (PAC) itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya siasa nchini,"
alisema.
Zitto alisema vyama vya siasa
vinatumia fedha za umma takribani sh bilioni 20 kila mwaka kama
ruzuku, kwamba ni haki ya wananchi kujua fedha zinatumika namna gani.
Alisema kuwa wananchi wa Nzega wana
changamoto nyingi sana.
Kwamba wakulima wa pamba walipewa madawa feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo
hovyo ni mingi mno na unyanyasi wa wana-CHADEMA ni mkubwa vijijini.
Chanzo: Mjengwa
No comments:
Post a Comment