Wanyonge walia, waporaji washerehekea
Siku ya leo nchi yetu inaadhimisha
miaka 14 tangu kuondokewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.Hivyo, leo ni siku ya furaha na huzuni; ni siku ya harusi na matanga.
Kwa waporaji, wanyonyaji, wabaguzi wa rangi, wadini na wakabila, leo ni siku ya
kunywa mvinyo na kusherehekea. Ule mwiba uliowachoma siku zote na kuwakosesha
raha hatimaye uliondoka siku kama ya leo, nao
wakapata nafasi ya kutamba.
Kwa wanyonge – wakulima wadogo,
wafugaji wadogo, warina asali, waokota makopo, wafagia barabara, wabeba zege,
machinga, mama ntiliye, wafanyakazi wa ngazi za chini, na wote wanaoishi katika
dhiki na kukosa huduma bora za afya, maji, elimu na malazi – leo ni siku ya
huzuni. Lile jabali lililoongoza mapambano yao
hatimaye lilistaafu rasmi kazi ya kupambana siku kama
ya leo. Nyerere, msemaji wa wanyonge, akaacha kusema. Kambarage, mshairi wa
makabwela, akaacha rasmi utunzi wa mashairi. Julius, mfasiri wa vitabu, akaweka
kalamu chini huku akiwa amekamilisha kutafsiri kwa Kiswahili kitabu cha
mwanafalsafa wa Kiyunani, Plato, kiitwacho ''The Republic''. Mwalimu wa
wanyonge akakoma kufundisha. Akatulia tuli. Akalala usingizi wa kudumu.
Tufurahie maisha yake kuliko
kuomboleza kifo chake
Je, ni sahihi kwa wanyonge kulia? Ni
haki kwa wanyonge kuomboleza? Kulia na kuomboleza ni haki ya kila ampotezae
mpendwa wake. Lakini kwa kuwa Nyerere alikuwa binadamu wa kawaida na sio
malaika aliyeshushwa toka angani hatukutegemea kwamba ataishi milele. Binadamu
huzaliwa, hukua, huzeeka, huugua, hufariki. Ndicho kilichotokea kwa Mwalimu.
Pengine siku ya leo yapaswa kuwa siku ya kufurahia maisha ya Mwalimu kuliko
kuhuzunikia kifo chake. Kwa maana hiyo, siku kama
ya leo twapaswa kuzitafakari kwa kina fikra zake na jinsi tutakavyozitumia
kuendeleza mapambano ya wanyonge.
Nyerere hajafa, sisi ndio Nyerere
Aina hii ya kumwenzi kiongozi wa mapambano kwa kuendeleza yale aliyoyapigania niliiona kwa Wavenezuela walipoondokewa na shujaa wao wa mapinduzi ya kidemokrasia, rais wa wanyonge, Hugo Chavez, alipofariki mwezi machi mwaka huu. Nilipowaona katika televisheni mamilioni ya wanyonge wa Venezuela wakitiririkwa na machozi, nilidhani huo ndio mwisho wa mapinduzi ya kijamaa ya kibolivari (The Bolivarian Socialist Revolution) waliyoyaasisi wanyonge wa nchi hiyo wakiongozwa Chavez.
Aina hii ya kumwenzi kiongozi wa mapambano kwa kuendeleza yale aliyoyapigania niliiona kwa Wavenezuela walipoondokewa na shujaa wao wa mapinduzi ya kidemokrasia, rais wa wanyonge, Hugo Chavez, alipofariki mwezi machi mwaka huu. Nilipowaona katika televisheni mamilioni ya wanyonge wa Venezuela wakitiririkwa na machozi, nilidhani huo ndio mwisho wa mapinduzi ya kijamaa ya kibolivari (The Bolivarian Socialist Revolution) waliyoyaasisi wanyonge wa nchi hiyo wakiongozwa Chavez.
Kilichonitisha zaidi ni jinsi
viongozi wa mataifa ya mabeberu, na hasa Barack Obama wa Marekani, walivyotoa
kauli za kusherehekea kifo cha gwiji hilo
la mapambano. Na mabeberu walikuwa na haki kushangilia kifo hicho kwani ni
Chavez aliyehakikisha kuwa utajiri wa mafuta ya nchi hiyo unaenda kuwafaidisha
wanyonge kwa kuwapatia hudumu bora za kijamii zisizo na malipo. Mawakala wa
ubeberu nchini Venezuela
wakisaidiwa na majasusi wa Marekani walijaribu kumpindua Chavez lakini
mamilioni ya wanyonge waliandamana hadi aliporejeshwa madarakani.
Lakini kauli za wanyonge wa Venezuela
zilinipa matumaini: pamoja na kutiririkwa machozi, walipohojiwa na waandishi wa
nchi za Magharibi juu ya kifo cha kiongozi wao, walijibu: ''Chavez hajafa. Sisi
ndio Chavez''. Kwa kauli hiyo wanyonge walikula yamini kuendeleza mapinduzi ya
kijamaa na kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi yao unaendelea kuwafaidisha wanyonge badala
ya kikundi kidogo cha mawakala wa mabeberu na mabwana wao.
Tena wanyonge wa Venezuela wameonyesha mshikamano wa kitabaka na
wanyonge wa nchi nyingine kama Cuba,
Ecuador, Nicaragua na Bolivia ambazo zote zinaongozwa na
serikali za kijamaa. Mathalani, Cuba yenye madaktari wengi waliobobea huwapeleka
Venezuela ili kutoa huduma
za afya kwa wanyonge mijini na vijijini, wakati Venezuela
ikiipatia Cuba
mafuta kwa bei rahisi na kuisaidia kiuchumi ili iondokane na hali ngumu
inayosababishwa na vikwazo vya Marekani.
Kambarage mpinga unyanyasaji
Historia ya Kambarage inaonyesha kuwa
tangu akiwa mdogo alichukia kila aina ya uonevu, ubaguzi, unyanyasaji na
ukandamizaji. Akiwa mtoto mdogo, Kambarage alikuwa akimsindikiza mama yake
shambani ; mama akiwa analima, Kambarage alikuwa akimbembeleza mdogo wake.
Huruma ilikiwa ikimwingia Kambarage kumwona mama yake akifanya kazi za suluba
siku nzima bila kupumzika.
Hivyo akabuni mbinu ya kumpumzisha mama yake. Akawa
anamfinya mdogo wake, na kitoto kile kichanga kikawa kikitoa kilio kikali,
kilio kilichomfanya mama adhani kuwa kichanga yule ana njaa. Hivyo, mama
akaacha kulima na kuja kumnyonyesha mwanawe. Kamnyonyesha mtoto, lakini pia
kapumzika. Kambarage alitabasamu na kujiona mshindi, hata kama
ushindi wenyewe ulikuwa wa muda mfupi tu.
Miaka mingi sana baadaye kitoto hiki, ki-Kambarage, sasa
akiwa kijana wa umri wa miaka 22 na mwanafunzi wa Makerere aliandika insha ya
kiswahili iliyoitwa ''Uhuru wa Wanawake''. Ndani ya insha hiyo kijana Julius
aliichambua na kuilaani mifumo ya jamii zetu za Kiafrika iliyokuwa
ikiwakandamiza na kuwanyanyasa wanawake kana kwamba wao si binadamu kamili. Na
ni mfumo wa kikoloni ulichochea moto na kuhalalisha mfumo dume.
Insha hiyo, ambayo ambayo ilishinda tuzo ya Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki kwa wakati huo, na sasa imechapwa katika kitabu, inaishia na kisa cha kifaranga cha tai kilichochanganywa na kuku, kikalishwa chakula cha kuku, hata chenyewe kudhani ni kuku. Lakini tai huyo alipopelekwa kilimani na mtaalamu wa wanyama, na kuambiwa: tai, wewe sio kuku, kwako ni angani, hivyo ruka uende angani. Tai akaruka na kupotelea mawinguni. Kwa kutumia mfano huo, Nyerere akawataka wanawake kutokubali madhila ya mfumo kandamizi unaowaaminisha kuwa wao ni kuku, warukia chini, ilhali wao ni tai, warukia juu. Hivyo walipaswa kuruka na kupaa.
Hata hivyo mtazamo wa Mwalimu haukuwa
finyu kwa kudhani kuwa ni wanawake pekee ndio waliokandamizwa na kunyimwa
fursa. Mfumo wa kibepari, ambao kwa wakati huo ulichukua sura ya ukoloni,
uliwakandamiza wanyonge wote, wake kwa waume, katika Afrika na mabara mengine.
Hivyo, wanyonge wote walipaswa kupambana na kuushinda ukoloni. Ndio maana
Nyerere alikuwa mbele kuongoza mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa rangi na
ukandamizaji, katika Afrika na dunia nzima kwa ujumla.
Julius asiyenunulika
Shuleni Tabora, Julius alipewa
ukiranja. Hii ilitokea baada ya yeye kuamua kuacha shule kutokana na
kunyamazishwa na mwalimu mkuu wakati wa mdahalo. Kambarage alikuwa ametoa hoja
za kupinga uonevu na unyonyaji wa serikali ya kikoloni hali iliyomwudhi mwalimu
mkuu wa kizungu na kumwamuru akae chini. Kwa nini anyamazishwe? Mwanafunzi huyo
aliamua kufunga virago vyake na kurudi kwao lakini utawala wa shule kwa
kushirikiana na serikali ya kikoloni walimkatiza na kumrudisha shuleni kisha
wakampatia uongozi.
Kama walimu wa kikoloni walidhani kwa
kumpa ukiranja walikuwa wamemnunua Julius basi walikuwa wakiota ndoto mchana
kweupe. Ukiranja wa shule ulimpa Kambarage haki ya kupata nusu lita ya maziwa
kila siku, ilhali wasio viranja walipata robo lita. Ni Kambarage, si mwingine,
aliyeongoza mgomo wa wanafunzi kupinga ubaguzi huo na kudai wanafunzi wote
wapate mgao sawa wa maziwa. Mgao huwa wa kibaguzi ukakoma. Tayari Nyerere
alishaanza kupigania usawa.
Miongo kadhaa baadae serikali ya
kikoloni ilimpatia ujumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika
(ubunge kwa wakati huo). Walidhani wamemnunua na kumnyamazisha. Lakini alipoona
hoja zake hazipewi nafasi Nyerere alijiuzulu ubunge huo na kuyarejea maisha
yake ya dhiki aliyokuwa akiishi baada ya kuacha kazi ya ualimu. Alikataa
kuwasaliti wanyonge.
Kipo kisa katika kitabu cha Mohamed
Said kiitwacho Uamuzi wa Busara wa Tabora kinachoonyesha maisha aliyoishi
Nyerere baada ya kuacha kazi ya ualimu iliyokuwa na mshahara mnono kwa wakati
huo ili kuongoza mapambano ya uhuru. Familia yake ikakosa hata mlo wa
kueleweka. Siku moja, akiwa hana hata senti moja mfukoni, Mwalimu aliamua
kutembea kwa mguu toka nyumbani kwake Magomeni hadi Kariakoo, akitegemea huenda
atabahatisha kupata chakula.
Njiani akakutana na mzee Msume Kiate, mwana TANU
ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza samaki. Baada ya kusikiliza shida ya
Mwalimu, mzee Kiate akampatia shilingi mia mbili akanunue mahitaji yake. Na
baada ya hapo mzee Kiate na wana TANU wenzake walijitolea kuihudumia familia ya
Mwalimu kwa chakula na wakaendelea kufanya hivyo hata baada ya uhuru
kupatikana. Tunapomkumbuka Nyerere tunapaswa pia kuwakumbuka mashujaa wengine,
kama Mshume Kiate, ambao vitabu vingi vya historia havitaji majina yao.
Mwalimu Nyerere, kiongozi wa
makabwela
Kitabaka, Mwalimu hakuwa katika kundi
la makabwela. Kwa kuzaliwa katika familia ya kichifu tayari alikuwa na fursa
ambazo watoto wengine hawakuwa nazo. Moja ya fursa hizo ilikuwa elimu. Lakini
elimu ikamfungua na kuiona dunia. Kadiri ilivyomfungua ndivyo ilivyomtenganisha
na watu wake. Toka Butiama akaenda Musoma, toka Musoma akapita Mwanza,
Shinyanga hadi Tabora. Akavuka mipaka ya kijiji na mikoa.
Akavuka mipaka ya
nchi, akaenda Uganda.
Akavuka mipaka ya bara, akaenda Uingereza. Elimu yake haikumvusha mipaka ya
ramani tu bali mipaka ya kitabaka. Kadiri alivyoongeza vidato na shahada ndivyo
alivyolihama tabaka la "walalahoi".
Lakini japokuwa kitabaka alikuwa
katika "walalahai" kabla ya uhuru, na kuhamia katika
"walalaheri" baada ya uhuru, Mwalimu mwenyewe aliamua kwa makusudi
kabisa kuliasi tabaka lake. Hivyo usomi wake haukuwa na bei (exchange value)
bali ulikuwa na thamani (use value). Katika fikra za Mwalimu, msomi anayejitapa
kuwa yeye hawezi kutumika kwa wanyonge mpaka alipwe kiasi fulani cha fedha huyo
si binadamu kamili bali ni mtumwa. Binadamu pekee mwenye bei na anayeuzika
sokoni ni mtumwa.
Ndio maana hata baada ya kutoka
Uingereza, akiwa Mtanganyika wa kwanza kupata shahada ya umahiri (master's
degree), Mwalimu hakuhangaika kutafuta fursa za kujitajirisha na kuishi maisha
ya anasa. Kwa kuwa maslahi hayo ya kitabaka alishayaaga haikuwa vigumu kwake
kuachia nyadhifa zenye malipo manono ili akawapiganie wanyonge.
Hata baada ya kukaa Ikulu kwa zaidi
ya miaka 20, alifanikiwa kujenga kajumba kadogo na ka kawaida kabisa kijijini
Butiama, na nyumba yake ya Msasani aliijenga kwa mkopo ambao hata hivyo
alishindwa kuumalizia, na kuiomba serikali imalizie mkopo na kuchukua nyumba
hiyo. Serikali ya Mwinyi ikafanya hivyo lakini ikampatia Mwalimu nyumba hiyo.
Mwaka 1966 Mwalimu alikata mshahara wake kwa asilimia 20.
Wakati huo alikuwa
akipokea shilingi 5,000/=, hivyo akabakia na shilingi 4,000/= na hakuwahi
kujiongezea mshahara mpaka anaondoka madarakani. Hivyo, wapo watumishi wengi
kabisa wa serikali, wakiwemo maprofesa, waliopokea mshahara mkubwa kumzidi.
Azimio liliwajali wanyonge
Lakini kutopenda mali inaweza kuwa hulka ya mtu yeyote kabisa. Mkristo au mwislamu mzuri, anayeamini katika pepo ya baadae, hawezi kujikita katika anasa za kidunia. Ila Nyerere alifanya hivyo si kwa sababu ya ukristo wake, ila kwa sababu ya itikadi iliyomwongoza, itikadi ya kijamaa. Ndiyo maana, baada ya kuwaona viongozi wenzake wanatumia nyadhifa zao kujitajirisha, aliasisi Azimio la Arusha, ambalo pamoja na mambo mengine liliwazuia viongozi kumiliki nyumba za kupangisha, kupokea mishahara miwili au zaidi na kumiliki hisa au kuwa wakurugenzi katika kampuni za kibepari.
Lakini kutopenda mali inaweza kuwa hulka ya mtu yeyote kabisa. Mkristo au mwislamu mzuri, anayeamini katika pepo ya baadae, hawezi kujikita katika anasa za kidunia. Ila Nyerere alifanya hivyo si kwa sababu ya ukristo wake, ila kwa sababu ya itikadi iliyomwongoza, itikadi ya kijamaa. Ndiyo maana, baada ya kuwaona viongozi wenzake wanatumia nyadhifa zao kujitajirisha, aliasisi Azimio la Arusha, ambalo pamoja na mambo mengine liliwazuia viongozi kumiliki nyumba za kupangisha, kupokea mishahara miwili au zaidi na kumiliki hisa au kuwa wakurugenzi katika kampuni za kibepari.
Kupitia Azimio la Arusha, njia kuu za
uzalishaji-mali na rasilimali za taifa, kama
viwanda, mabenki, misitu, madini, ardhi, njia na vyombo vya usafiri wa anga,
reli na maji, viliwekwa mikononi mwa umma. Umma wa wanyonge ulichagua serikali
kwa njia ya kidemokrasia, serikali ambayo ilipewa jukumu la kusimamia
rasilimali hizo kwa niaba ya wanyonge. Faida inayozalishwa ilitakiwa kwenda
kuwahudumia wanyonge, na sio kikundi cha watawala. Azimio lilisisitiza juu ya
kuwajali wakulima vijijini, na kuonya juu ya misaada kutoka ughaibuni.
Azimio likahujumiwa na kupinduliwa
Kama inavyofahamika, wanyonge, wake kwa waume, vijana kwa wazee, waliandamana nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha. Lilikuwa ramani yao kuelekea nchi ya usawa na matumaini. Lakini hata hivyo, utekelezaji wa Azimio uliwekwa mikononi mwa watu walewale walioanza kujitajirisha. Japo katika miaka ya 1970 sera za kijamaa zilifanya vema na serikali ikaanza kuonyesha mafanikio katika kutoa hudumu bora kwa jamii bila malipo, hali ilibadilika katika kipindi cha miaka ya 1980.
Kama inavyofahamika, wanyonge, wake kwa waume, vijana kwa wazee, waliandamana nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha. Lilikuwa ramani yao kuelekea nchi ya usawa na matumaini. Lakini hata hivyo, utekelezaji wa Azimio uliwekwa mikononi mwa watu walewale walioanza kujitajirisha. Japo katika miaka ya 1970 sera za kijamaa zilifanya vema na serikali ikaanza kuonyesha mafanikio katika kutoa hudumu bora kwa jamii bila malipo, hali ilibadilika katika kipindi cha miaka ya 1980.
Nchi za kibeberu, Marekani na
Uingereza, zilishikwa na waumini wa sera za uliberali mambo-leo na hivyo kuzilazimisha
nchi maskini kufuata sera hizo kwa kubinafsisha kila kilichotaifishwa, kufuta
ruzuku katika kilimo na vyakula, na kuacha mara moja kutoa huduma zisizo na
malipo. Ndani ya nchi, tena Mwalimu akiwa bado madarakani, sera hizi zilipata
mashabiki wengi. Wachache walijionyesha waziwazi. Wengi walijificha na
kuendelea kuhujumu chini chini.
Nchi ikiwa imetoka vitani, bidhaa za
msingi zikawa hazipatikani. Zilikuwa zimehodhiwa na kikundi cha watu wachache,
baadhi wakiwa katika dola na baadhi nje ya dola. Hivyo, baada ya vita vya Uganda, Mwalimu
alikuwa na vita viwili vya kupigana: vita dhidi ya wahujumu uchumi/ujamaa ndani
ya nchi, na vita dhidi ya mabeberu nje ya nchi. Makundi hayo yalikuwa
yakishirikiana kwa ukaribu sana,
na hata yakafanikiwa kuupindua Ujamaa baada ya Mwalimu kung'atuka.
Sera za kiporaji
Uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ya
utekelezaji wa sera za uliberali mambo-leo umetuonyesha kuwa mfumo huu ni
katili zaidi pengine kuliko hata biashara ya utumwa na ukoloni. Rasilimali za
wanyonge zinaporwa, na wanyonge wanapojaribu kupinga hutumiwa majeshi na
serikali zao au za mabeberu. Tumeyaona hayo nchini mwetu. Pia tumeyaona barani
kwetu na duniani kote mifano ikiwa ni uvamizi wa Libya
na Iraq
uliopelekea kuchinjwa kwa viongozi wa nchi hizo, na mamilioni ya wanyonge
kuuawa.
Akihutubia mjini Mbeya katika sherehe
za Mei Mosi mwaka 1995, Mwalimu aliziita sera za ubinafsishaji na uwekezaji
kuwa ni za kinyang'anyi. Akasema kuwa zitazalisha mabilionea, lakini watakuwa
wachache. Lakini pia zitazalisha maskini, na hao watakuwa wengi sana. Hayo ndiyo
yatokeayo nchini mwetu na duniani kote.
Jengeni sanamu zake, sisi tutazienzi
fikra zake
Mwaka mmoja kabla ya kufariki Mwalimu alikuwa ametabiri kuwa ipo siku Tanzania itarejea katika misingi ya Azimio la Arusha. Katika Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha, Profesa Issa Shivji naye pia alisisitiza juu ya uwepo wa dalili zinazoonyesha kuwa Watanzania walio wengi wameanza kupigania kurudi katika misingi ya Azimio la Arusha lakini akaonya kuwa dalili hizo zinaweza kuzimwa na kakundi ka watu wachache kanakofaidika na mfumo uliopo.
Mwaka mmoja kabla ya kufariki Mwalimu alikuwa ametabiri kuwa ipo siku Tanzania itarejea katika misingi ya Azimio la Arusha. Katika Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha, Profesa Issa Shivji naye pia alisisitiza juu ya uwepo wa dalili zinazoonyesha kuwa Watanzania walio wengi wameanza kupigania kurudi katika misingi ya Azimio la Arusha lakini akaonya kuwa dalili hizo zinaweza kuzimwa na kakundi ka watu wachache kanakofaidika na mfumo uliopo.
Nafikiri kuwa miongoni mwa mbinu za
kuzima dalili hizo ni kuhodhi jina la Mwalimu huku wakijidai wanamuenzi. Eti
wanamuenzi kwa kuongeza idadi ya sanamu zake, na taasisi na viwanja vyenye jina
lake ilhali Mwalimu mwenyewe alishakataa hayo
tangu akiwa hai. Wakijidai kugusia fikra zake basi wanamhubiri kama mpenda amani na umoja. Lakini ni Mwalimu mwenyewe
aliyesema kuwa mahali pasipo na haki (justice) wala usawa (equity) hapawezi kuwa
na amani. Pia hauwezi kuwa na umoja kati ya wanyonyaji/waporaji wachache na
mafukara wengi.
Ili nisionekane nabandika maneno katika
mdomo wa Mwalimu, nitanukuu sehemu ya hotuba yake aliyoitoa mwezi mei mwaka
1989 wakati akifungua semina ya wazalishaji wakubwa iliyoandaliwa na Chama cha
Mapinduzi:
"Si kwamba Azimio la Arusha
limeondoa umaskini hata kidogo, wala halikutoa ahadi hiyo. Azimio la Arusha
limetoa ahadi ya matumaini. Ya haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio watu
wengi wa Tanzania
wanaendelea na kuwa na matumaini hayo. Madhali yapo matumaini hayo, mtaendelea
kuwa na amani... Kama wengi hawana matumaini,
tunajenga 'volcano'. Siku moja italipuka na lazima ilipuke. Isipokuwa watu hao
wajinga.
Wengi wa nchi hiyo wajinga, wanakubali kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa
hivi hivi na wingi wanao, wajinga hao. Kwa hiyo, Watanzania hawa watakuwa
wajinga, wapumbavu, kama wataendelea kukubali kuonewa na watu wachache katika
nchi yao. Kwa
nini?''
Waporaji wa rasilimali za nchi,
wavunaji wa jasho la wanyonge, vibaraka wa mabeberu (wasemao 'tunapendwa huko
nje') hawana haki ya kutumia jina la Mwalimu.
Wametupora kila kilicho chetu
(tangu viwanda, ardhi, madini hadi nyumba), wamewanyang'anya wanyonge haki ya
kupata huduma bora za afya, elimu, malazi na chakula. Hawa hawana haki ya
kutaja jina la Mwalimu. Njia ambayo wanyonge wanaweza kumuenzi Mwalimu ni kwa
kuzichambua kwa kina fira zake, na hasa Azimio la Arusha, na kuzitumia kama silaha ya mapambano!
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com
Source: http://www.wavuti.com/
No comments:
Post a Comment