Wednesday, October 30, 2013

WABUNGE WAILALAMIKIA SERIKALI




Baadhi ya wabunge , wameitupia lawama Serikali baada ya kutoridhishwa na majibu wanayopewa juu ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukomesha vitendo vya ujangili wa wanyama jambo linaloweza kuua sekta ya utalii nchini.

Hali hiyo ilijitokeza bungeni Mjini Dodoma jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo baadhi ya wabunge walitaka Serikali itoe taarifa sahihi za ukubwa wa tatizo hilo na kuwataja wahusika badala ya kunyamaza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Bw. William Lukuvi, alisimama na kutoa ufafanuzi wa kina juu ya hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua kukabiliana na biashara haramu ya meno ya tembo.
Alisema tayari imeundwa timu inayofanya Operesheni Maalumu ya kupambana na kuwabaini wahusika wa biashara hiyo hivyo ni mapema sana kuwataja kwa sasa.

"Watu wanaotuhumiwa ni wengi, hata msaidizi wangu jimboni alikamatwa akiwa ofisini na kupigwa akihusishwa na biashara hiyo ila baadaye walimuachia baada ya kujiridhisha.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, alisema suala la ujangili si la kufanyiwa mzaha kutokana na athari zake kuwa kubwa.

"Hapa hakuna kulindana, mtu yeyote ambaye itabainika anahusika na biashara ya meno ya tembo, tutamkamata na kumchukulia hatua za kisheria," alisema Bw. Nahodha.
Aliwataka wanasiasa kutoingilia suala hilo kwani zipo taarifa za baadhi yao kutumia nguvu ya siasa ili kuwatetea wahalifu kwani Serikali haina mzaha na jambo hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bw. James Lembeli, alidai kuwa wapo baadhi ya makamanda walioko maeneo mbalimbali ya nchi ambao wanajihusisha na vitendo vya ujangili.

Aliitaka Serikali itoe ufafanuzi kwanini inashindwa kuwachukulia hatua za kisheria badala yake wanaendelea kuwafumbia macho.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu, alisema hadi sasa wapo maofisa wa vyombo vya usalama wanashikiliwa polisi kwa tuhuma za ujangili.

Bw. Nyalandu aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Dar es Salaam, Bw. Faustin Ndungulile juu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti janga hilo nchini.
Alisema Serikali haitawavumilia makamanda na wanasiasa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili hasa mauaji ya tembo ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotisha kwa biashara haramu ya meno yake.

"Hali hii inachangiwa na Serikali kuwa na uhaba wa askari wanyamapori anayepaswa kulinda umbali wa kilomita 25 tofauti na zamani alikuwa akilinda kilomita za mraba 150,000.
"Serikali ina mpango wa kuyatenga maeneo yanayofaa kuwa vitaru kutokana na malalamiko yaliyopo kuwa vinatumika kuwindia tembo kitendo ambacho ni kinyume cha sheria," alisema.

Awali Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema, alidai waliopewa vitalu pembezoni mwa hifadhi za wanyama huvitumia kuwaua wanyama ambao wanakatazwa kuwindwa kisheria

No comments: