Wednesday, October 30, 2013

Tanzania: Tunaweza kujitoa A. Mashariki



Serikali ya Tanzania imesema inatafakari ushiriki wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na inaweza kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo itaendelea kutengwa katika baadhi ya vikao.

Aidha imesema Tanzania haitambui vikao vinavyofanywa na nchi tatu zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikizitenga Tanzania na Burundi.
Waziri anayehusika na masuala ya Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta ameliambia Bunge la Tanzania kuwa makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na nchi za Kenya, Rwanda na Uganda yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao hivyo kwa sababu vinafanyika nje ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo.
Katika mikutano iliyofanyika hivi karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa kwenye vikao hivyo.

Kwa mujibu wa Waziri Sitta mikutano ya wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambayo ilianza kwa kuitenga Tanzania ilifanyika Entebbe nchini Uganda mwezi Juni mwaka huu na kufuatiwa na mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka huu huko Mombasa nchini Kenya ambapo nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania walizungumzia uanzishaji wa himaya moja ya forodha.

Mambo mengine waliyozungumza wakuu hao ilikuwa uanzishaji wa visa moja ya utalii kwa nchi zao na matumizi ya vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika kama hati za kusafiria miongoni mwa nchi hizo.
Aidha Waziri Sitta amesema ndani ya mikutano hiyo pia walizungumzia kuanzisha mchakato wa kuanzisha shirikisho la nchi hizo.

Tayari Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuangalia ni kwa namna gani zitaanzisha ushirikiano nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama zinavyofanya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya.
Tanzania imesema itatoa msimamo wake wiki hii kuhusu mkutano wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ngazi ya marais, uliotarajiwa kufanyika jana kujadili masuala yanayohusu maslahi ya nchi zilizoko katika ukanda huo bila kushirikishwa.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, aliliambia NIPASHE mjini hapa jana kuwa mkutano huo ulitarajiwa kufanyika nchini Rwanda jana na kwamba ungehusisha marais wa nchi za Rwanda, Paul Kagame; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la NIPASHE lililotaka kauli ya serikali kuhusu uamuzi wa nchi hizo kuendeleza tabia yao ya kuitenga Tanzania katika mikutano yao.

"Mkutano wa Rwanda unafanyika leo ngazi ya marais. Tunasubiri kupata maazimio. Tanzania itatoa msimamo wiki hii," alisema Waziri Sitta bila kutaka kuingia kwa undani kuhusiana na suala hilo.

Mkutano huo ni wa tatu kufanyika bila kuishirikisha Tanzania. Mara mbili mfululizo, marais wa nchi hizo walikutana na kujadili mchakato wa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo, huku wakiitenga Tanzania.

Marais Kenyata, Museveni na Kagame alikutana mara zote hizo bila kumualika Rais Jakaya Kikwete.Kwenye vikao viwili vilivyofanyika nchini Uganda na Kenya, viongozi hao walikubaliana kutekeleza kwa haraka miradi ya ujenzi wa reli itakayounganisha nchi hizo na bomba la mafuta litakalojengwa kuanzia Sudan Kusini hadi Mombasa na lingine kutoka Kenya hadi Rwanda.

Pia nchi hizo zilitangaza kuanzia Januari Mosi, raia wao watembeleane bila kuwa na hati za kusafiria, pia kuwa na viza moja kwa watalii.
Mkutano wa Kenya ulioambatana na ufunguzi wa gati katika bandari ya Mombasa, nchi za Burundi na Sudani Kusini zilialikwa na kuwakilishwa na mawaziri wao waandamizi, lakini Tanzania haikualikwa.

Vile vile, vyombo vya habari viliwakariri baadhi ya mawaziri wa nchi hizo waliopewa jukumu la kusimamia makubaliano hayo, wakiyaeleza kuwa ni ya jumuiya nzima na endapo Tanzania ikipenda kuingia itakaribishwa. Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania ilionyesha wasiwasi wake juu ya mwenendo wa nchi hizo.

Ilipinga dalili zinazoonekana kwa nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kutumia jina la EAC kuomba fedha au kugharimia miradi inayopaswa kuwa ya jumuiya.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Abdullah Juma Saadalla.

Alisema malalamiko hayo yalishawasilishwa pia katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa EAC, kilichofanyika jijini Arusha.
Dk. Saadalla alisema serikali imemtaka Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, kutoa maelezo juu ya gharama ya miradi kadhaa inayoaminika kuwa sehemu ya jumuiya hiyo. Pia alisema hatua zilizochukuliwa na nchi hizo kwa kukubali kuanzisha utaratibu wa matumizi ya viza moja na vitambulisho vya pamoja, ni mfano wa ubabe usiokidhi matakwa ya kidemokrasia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hivi karibuni kuwa Tanzania ikibaini kuwapo haja ya kujitoa EAC itafuata utaratibu kwa kulifikisha suala hilo bungeni ili wabunge waliamue.
Chanzo: BBCSwahili/Nipashe

No comments: