Friday, October 25, 2013

Dk. Nchimbi airarua ripoti ya uhalifu




Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi ameirarua ripoti ya uhalifu na kusema kuwa waliofanya kazi hiyo wana lao jambo. Mbali na hilo, Dk. Nchimbi, amesema kuwa anashangazwa na utafiti huo ambao umeilenga Tanzania pekee ambayo lengo lake ni kutaka kuua biashara ya utalii, kwa kujenga hofu miongoni mwa jamii na taasisi za kimataifa.


Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Taasisi ya Utafiti kuhusu kuondoa Umasikini (REPOA), kutangaza matokeo ya uhalifu, ambapo walibaini kuwa Tanzania ni kinara wa matukio ya kihalifu katika nchi za Afrika.

Akizungumza na RAI jana katika mahojiano maalumu, Dk. Nchimbi alishangazwa na ripoti hiyo kushindwa kuona hali ya usalama katika nchi ya Kenya ambayo hivi karibuni ilivamiwa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab ambao walifanya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema kuwa anashangazwa na ripoti hiyo kutoa asilimia kumi hali ya kuwa matukio ya kihalifu yameshamiri kila kona ya nchi.

“Ukiangalia kwa upande wa usalama wa matukio ya kihalifu kwa nchi za Kenya na Uganda, sisi tuko salama kabisa, lakini matukio yao hayatangazwi kwanini ya nchini kwetu tu ambayo kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuyathibiti,” alisema.

“Lakini tukio la hivi karibuni ambalo kuna vijana 11 waliokamatwa msituni kwa kudaiwa kuwa walikuwa wakifanya mafunzo ya kigaidi kwa kutumia CD za Al Qaida na Al Shabaab, nchi jirani walilitangaza kila kona ya dunia.

“Wanafanya hivi kuipaka matope nchi yetu kwa makusudi ili watalii waende kwao, lile tukio la Mtwara walilitangaza dunia nzima na kila balozi nilizotembelea waliohoji, iwapo wako salama na raia wao?” alisema na kuhoji Dk. Nchimbi.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa hawezi kuizungumzia ripoti ya REPOA kwa sababu hajaisoma kwa undani huku akisema ni wazi ina lengo la kutaka kuwatia hofu watalii na wananchi ambao aliwataka wawe huru kwani wako salama.
Kauli ya Jeshi la Polisi
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limewataka wananchi kutotishwa na matokeo ya utafiti huo.

Msemaji wa jeshi hilo, SSP Advera Senso, alisema matokeo hayo yana lengo la kufifisha juhudi za wananchi na vyombo vya usalama nchini, katika kudhibiti na kupambana na uhalifu.

Senso, alisema matokeo hayo yameangalia namna vyombo vya usalama nchini vilivyofanikiwa kukamata wahalifu kwa msaada wa wananchi.

SSP Senso alisema ripoti hiyo imethibitisha juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kuwafundisha wananchi namna ya kukabiliana na kudhibiti matukio ya uhalifu.

“Ukamataji wahalifu umeongezeka baada ya wananchi kuwa na ‘awareness’ kubwa, wanadhibiti zaidi ndio maana wao wanasema uhalifu umeongezeka, lakini siyo kweli,” alisema SSP Senso.

SSP Senso alisema Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Afrika iliyofanikiwa kupambana na kudhibiti uhalifu wa mipaka inayokwenda nchi nyingine.

“Leo hii hatukubaliani na utafiti huo, mkutano wa machifu (IGP), uliofanyika 2011, tulipewa sifa kubwa kuwa ni nchi ya kwanza barani Afrika tumefanikiwa kupambana na uhalifu mipakani.

“Hivi ndivyo viashiria tunavyotumia kujifunza vizuri, tunapowakamata wahalifu watu wengine wasiseme uhalifu umeongezeka,” alisema Senso.

Utafiti huo wa REPOA, yameonyesha kuwa vitendo vya watu kujeruhiwa kutokana na uhalifu vimeongezeka nchini, huku idadi ya watu waliojeruhiwa imeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2003 hadi asilimia 44 mwaka 2012.

Kwa upande wa watu walivyo na hofu ya kuibiwa kwenye nyumba zao, ripoti hiyo ilionyesha kuwa vitendo vya kihalifu viliongezeka kuanzia mwaka 2008 na mwaka 2003 kulikuwa na matukio mengi kwa asilimia 48, lakini mwaka 2005 yakapungua hadi kufikia asilimia 34.

“Ufike wakati Watanzania tuwe wazalendo kama watu wanaona upo mwanya wa kuwapo matukio ya kihalifu, ni vyema waripoti kwenye vyombo vya usalama na yatafanyiwa kazi kwa upana wake.

“Wakati mwingine haya mashirika na watu hawajui athari ya haya wanayoyatangaza, hayaisadii nchi na raia wake,” alisema Waziri Nchimbi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya REPOA, asilimia 40 ya wananchi 2,400 waliohojiwa wana hofu ya kufanyiwa uhalifu na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kinara kati ya nchi 34 zilizofanyiwa utafiti huo.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa kati ya Mei hadi Juni, 2012 kwa kushirikiana na Asasi ya Afrobarometer, ililenga kuchunguza hali ya uhalifu nchini na utayari wa wananchi kutoa taarifa za kihalifu kwa polisi.

No comments: