Sunday, October 27, 2013

Sumaye amemtaka JK Kuchukua hatua



na Mwandishi wetu
SIKU mbili baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli ya kuhofia chama chake kuondoka madarakani iwapo rushwa itashindwa kutokomezwa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amemtaka kiongozi huyo kuchukua hatua.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana, Sumaye alisema kuwa wala rushwa wanajulikana, lakini wameshindwa kuchukuliwa hatua.

Sumaye alisema kuwa anashukuru Rais Kikwete kubaini tatizo hilo na kumshauri kwenda mbali zaidi, ikiwa ni pamoja na kulifanyia kazi na kuwachukulia hatua watu hao.
“Kama rais naye amegundua hilo, basi ni vizuri zaidi, ayafanyie kazi hayo. Msimamo wangu unajulikana, nimeshalalamika sana kuhusu rushwa, najua rushwa inakwamisha maendeleo, tuchukie rushwa, tutafute nafuu ya maisha kwa Watanzania wote, sio nafuu ya mtu mmoja mmoja,” alisema.

Alipoulizwa na gazeti hili kama anawajua wala rushwa na hatua ambazo anamshauri rais achukue, Sumaye alisema kuwa watu hao wanajulikana na wameshawahi kuandikwa, hivyo hana haja ya kuwataja.
“Wanajulikana, kama na ninyi mmeshawaandika basi wanajulikana, sina haja ya kuwataja,” alisema.

Waziri Mkuu huyo mstaafu, mwaka jana alilalamikia rushwa baada ya kuenguliwa katika kuwania ujumbe wa NEC katika Wilaya ya Hanang ambako Mary Nagu aliibuka kidedea.
Siku za hivi karibuni, Sumaye alikaririwa akisema wanaokerwa na karipio lake kuhusu rushwa, wanapaswa kuachana na vitendo hivyo viovu.
Sumaye, alitoa karipio hilo kwa viongozi wa dini, hususani ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), akionya kuhusu kasi ya wanasiasa kutumika katika harambee zake.

Alikaririwa akisema miongoni mwa wanasiasa hao, wanatumia mwanya huo kama njia ya kuungwa mkono watakapotangaza kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ingawa hakuwataja wanasiasa hao kwa majina, kauli yake ilitafsiriwa kumgusa aliyekuwa mrithi wake, Edward Lowassa, ambaye baadaye alijiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond.
Lowassa, mbunge wa Monduli, ameshiriki harambee mbalimbali nchini, hali inayoelezwa na baadhi ya wachunguzi wa mambo ya siasa kuwa na lengo la kujisafishia njia kuelekea katika kinyang’anyiro cha urais wa 2015.

Lakini Lowassa amekanusha kushiriki harambee hizo kwa nia ya kutafuta urais, badala yake akasisitiza kwamba ana karama ya ushawishi inayomfanya afanikishe shughuli hizo kwa kupata fedha nyingi.

Naye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja, alisema anamuunga mkono Rais Kikwete kwa kuwa rushwa imeumiza taifa, imepoteza rasilimali nyingi, na ufisadi mkubwa umepitia hatua iliyosababisha maendeleo kurudi nyuma.
“Suala la rushwa linaaibisha taifa letu, tusilitazame kama suala la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, tulitazame kama suala la Watanzania wote, tuchukie rushwa, rushwa itazamwe kwa mapana yake, na kila Mtanzania ajue madhara ya rushwa, hapa ndiyo tutasaidia taifa,” alisema.

Alisema kuwa kama rushwa itaendelea kushamiri, haki za wananchi zitaminywa, huduma za muhimu hazitapatikana kwa njia ya haki, hivyo wananchi wataendelea kuteseka na kukosa huduma hali ambayo inasababisha watu kuichukia CCM na serikali yake.
Ngeleja alisema kuwa anamuunga mkono Rais Kikwete kwa kauli yake, na kuwataka Watanzania wazidishe mapambano dhidi ya rushwa, na wenye ushahidi kwa watuhumiwa wa rushwa wajitokeze ili kuisaidia Takukuru ifanye kazi yake ipasavyo.

Aidha, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama alisema Rais Kikwete anaonekana sasa kuwa na nia nzuri na taifa, hivyo alimuomba Mungu amsamehe makosa ya zamani, kwa kuwa msimamo wake wa sasa unaitesa CCM.

“Kauli ya Kikwete ya sasa imenifanya nifikirie uamuzi wa kuendelea kulipia kadi yangu ya CCM, kwani niliacha tangu 2005, baada ya kuona chama kinaendeshwa kwa rushwa. Mimi ninampongeza kwanza kwa kukiri yale ambayo yalitufanya tuache kulipia kadi, sasa tunamhimiza afikirie zawadi ya MO Ibrahim, asimamie upatikanaji wa katiba mpya kwa njia ya haki na kusikiliza maoni ya wapinzani, atusaidie kusimamia uchaguzi wa mwaka 2015 bila rushwa, hayo yataandika historia nzuri ya jina lake na atakumbukwa kwa msimamo huu,” alisema.

Chanzo: Tanzania daima

No comments: