Thursday, October 31, 2013

Abwao amshika pabaya Lukuvi




na Salehe Mohamed, Dodoma
UTARATIBU wa mawaziri kuwa wabunge jana ulionesha udhaifu wake baada ya kusababisha mvutano mkubwa bungeni kati ya Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (CHADEMA), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Mvutano huo ulitokea baada ya Abwao anayetoka Mkoa wa Iringa kuuliza swali la uhaba wa maji katika Jimbo la Isimani linaloongozwa na Lukuvi.
Abwao alilielekeza swali hilo kwa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), akitaka kufahamu ni lini vijiji vilivyomo katika Jimbo la Isimani vitapata huduma ya maji safi na salama.

Wakati akiuliza swali hilo wabunge kadhaa walikuwa wakipiga makofi kumshangilia, hali iliyomfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtaka aliulize tena, kwa madai kuwa hakulisikia.
Mbunge huyo alilazimika kulirudia swali hilo ambalo lilijibiwa na Waziri Stephen Wassira, ambaye alisema tatizo hilo si la Isimani pekee bali ni la nchi nzima na kwamba serikali itahakikisha vijiji vyote vinapata maji.

Baada ya Wassira kutoa jibu hilo, Lukuvi alisimama kushibisha majibu ya waziri mwenzake, lakini baadhi ya wabunge walikuwa wakipiga kelele kupinga uamuzi wake huo.

Licha ya kelele hizo, Spika alimpa nafasi ya kuzungumza, akimtaka azungumze kama mbunge lakini Lukuvi alisema angelizungumza kwa kofia ya uwaziri.
“Mimi ni waziri, ninaweza kuzungumzia jambo la wizara yoyote ile, hivyo hawa wenzangu wanaona nimekiuka kanuni, wanakosea, nataka waelewe vizuri mambo haya,” alisema.

Lukuvi alisema serikali inafahamu tatizo la maji la jimbo hilo na inatekeleza mradi wa sh bilioni tatu huku mbunge wake (yeye) akishiriki kikamilifu kutafutia ufumbuzi.
Alibainisha kuwa tayari vimekwisha kuchimbwa visima 25 vya maji kwa jitihada zake binasfi na mpango mwingine wa kuchimba visima vingine 10 unaendelea.
“Mipango hii yote ikikamilika kila kijiji kitakuwa na uhakika wa maji pamoja na kuwa na kisima kimoja cha akiba,” alisema.

Majibu hayo ya Lukuvi yalizusha vifijo na kuzomeana ndani ya Bunge kulikokwenda sambamba na kurushiana maneno baina ya wanaomuunga mkono na wale wa Abwao, ambao walidai kuwa ana masilahi na Jimbo la Isimani.
Mara baada ya Lukuvi kumaliza kutoa ufafanuzi wake huo, Makinda alisema kuwa kila mbunge ana haki ya kutoa maelezo juu ya jimbo lake anapoona kuna mwenzake kalizungumzia.

Hata hivyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alisimama na kuomba mwongozo kuhusiana na hatua hiyo ya Lukuvi kutumia kofia mbili kujibu swali ambalo hakuulizwa.

Akitumia kanuni ya 68 (7), Mnyika alihoji sababu ya Lukuvi kusimama na kutumia mamlaka ya ubunge kujibu hoja hiyo wakati yupo kwa ajili ya nafasi ya uwaziri.
“Nimesimama kwa kanuni ya 68 (7), wakati wa kipindi cha maswali alisimama Mheshimiwa Lukuvi kujibu swali la Mheshimiwa Abwao, lakini alijibu akitumia cheo chake cha ubunge, wakati kanuni ya 39 (1) inatoa ruhusa kwa waziri kujibu maswali na hoja za wabunge na si wabunge.

“Kanuni ya wabunge kujibu maswali inahusu wabunge walioulizwa na walioteuliwa kwa kazi maalumu, kilichotokea leo inaonyesha wazi kuwa mchanganyiko wa vyeo unaleta madhara, waziri atakiwe kuepuka kutumia nafasi; nilikuwa naomba mwongozo wako,” alisema Mnyika.
Katika mwongozo wake, Makinda alisema Lukuvi yuko sahihi mpaka hapo Katiba itakapotenganisha kofia ya ubunge na uwaziri.

Utoro wa mawaziri
Katika hatua nyingine, kumejitokeza tukio la kushangaza la mawaziri wengi kutokuonekana bungeni wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015, hatua iliyowafanya wabunge wakiongozwa na Spika Anne Makinda kuwashambulia kwa utoro.

Juzi jioni wakati akiahirisha mjadala huo, Makinda aliwaonya baadhi ya mawaziri kuwa kutokuwapo kwao bungeni kutaiathiri serikali katika kujibu hoja za wabunge.
“Nyinyi mawaziri msidhani huu mjadala na mpango huu unamhusu Waziri Wassira peke yake…hapana, huu unahusu wizara zote, maana litaulizwa swali ambalo Wassira hana jibu lake, lazima muwepo,” alisema.

Licha ya onyo hilo, jana hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo mawaziri na manaibu waliokuwapo ndani ya ukumbi idadi yao ilikuwa haizidi saba wakati baraza zima wako zaidi ya 50.

Kutokana na utoro huo, wabunge wengi waliochangia mjadala walisema utoro huo umesababisha kutowajibika ipasavyo, hivyo maendeleo kusuasua.
Waliongeza kuwa utoro huo unadhihirisha dharau walizonazo na kwamba hao ndio kikwazo cha mipango mizuri inayoandaliwa na serikali.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema serikali inaonesha ina mchoko mkubwa ndiyo maana mawaziri waliomo ndani ya Bunge wakifuatilia mjadala huo hawazidi wanne.

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, alisema haoni kama mpango huo utafanikiwa kwa kuwa wasimamizi na watekelezaji wa mpango huo hawapo bungeni.
Kombo Hamis Kombo (CUF), alisema mawaziri na manaibu wao wanafanya mchezo wa kuigiza katika mambo muhimu kwa taifa, badala ya kuweka mkazo kwenye kusikiliza mapendekezo ya wabunge kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Kutokana na mashambulizi hayo, Waziri asiye na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliwakingia kifua mawaziri na manaibu wao akisema wanafuatilia mijadala hiyo kupitia runinga.

Aliongeza kuwa kutokuwapo kwao na watendaji wengine bungeni si kikwazo cha utekelezaji wa mpango huo, kwa kuwa serikali inafanya kazi kwa njia mbalimbali, ikiwamo hiyo ya runinga.
Waziri huyo alisema kila kinachosemwa bungeni kinaandikwa na maofisa wa serikali ambao hukifikisha katika ngazi husika kwa ajili ya utekelezaji zaidi.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: