Wednesday, October 30, 2013

Mbunge Kilombero akalia kuti kavu



Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wamemlalamikia Mbunge wa Kilombero, Abdallah Mteketa, kwa madai ya kutoshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Ilani ya chama hicho jimboni kwake.

Aidha, wajumbe hao wamedai kuwa mbunge huyo anafanya kazi zake za ubunge kwa chini ya asilimia 40 tu.
Walitoa kauli hiyo juzi baada ya kukutana na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Morogoro ambapo baadhi yao walidai mbunge huyo kutoonekana jimboni na kushindwa kushiriki vikao vya baraza la madiwani.
Walisema kitendo hicho kinawafanya wananchi kukilalamikia chama hicho kwa kukosa uwakilishi.

Walidai kuwa mbunge huyo amekuwa akiwaweka viongozi wa wilaya hiyo katika wakati mgumu kutokana na kushindwa kujibu maswali wanayoulizwa na wananchi wake juu ya kero mbalimbali, wakati kazi kubwa ya mbunge ni kuchukua kero za wananchi na za kijamii na kuziwasilisha bungeni zitafutiwe ufumbuzi.

Alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo, Mteketa alidai kuwa viongozi wa wilaya hiyo ndiyo wamekuwa chanzo cha kukwamisha utendaji wa kazi zake kutokana na kutompa ushirikiano pale anapohitaji kutekeleza masuala ya kisiasa.
Aidha, alidai kuwa hata anapoomba ushirikiano wao kwenda kwenye shughuli za wananchi, hudai hawana nafasi huku akitaja sababu nyingine kuwa ni kuuguliwa na mkewe aliyepooza.

Aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo akiwamo Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho wilaya, kwamba hawakumtaka hata wakati alipokuwa akiwania nafasi hiyo ya ubunge.
Hali kadhalika, alisema bado wameendeleza makundi yaliyotokana na uchaguzi baada ya kushinda na badala yake wamekuwa wakitengeneza wabunge wao watarajiwa kinyume na utaratibu wa CCM.

Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Rodgers Romuli, alithibitisha kupokea malalamiko hayo, ingawa jukumu lao kama chama ni kumwita na kumwambia yaliyojitokeza ili ayafanyie kazi kwa manufaa ya chama hicho.
CHANZO: NIPASHE

No comments: