Tuesday, October 29, 2013

AZAM YAIONJESHA SIMBA LAMBALAMBA




Simba jana ilionja machungu ya kufungwa katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-1na Azam FC katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa.
Kwa matokeo hayo Azam sasa inaongoza ligi hiyo kutokana na kujikusanyia pointi 23,huku ikiiacha Simba nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 20 wastani mzuri wa mabao ya kufungwa na sawa na Mbeya City yenye pointi 20 lakini imezidiwa mabao.

Mpira ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu ambapo Simba ilipata bao dakika ya 21 kupitia kwa Ramadhan Singano 'Messi' baada ya kupokea pasi ya Zahoro Pazi.
Azam nayo ilisawazisha bao hilo dakika ya 40 lililofungwa na Kipre Tchetche baada ya kuunganisha krosi ya Erasto Nyoni na kumuacha kipa wa Simba, Abel Dhaira akichupa bila mafanikio.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam ku fanya mashambulizi ambapo dakika ya 47 ,Kipre Tchetche aliachia shuti kali lakini likatoka nje ya lango.
Dakika ya 60 Simba ilikosa bao la wazi ambapo Mombeki,alifumua kombora kali akiwa nje ya 18 lakini likatoka nje ya lango la Azam.
Azam ilijibu shambulizi hilo dakika ya 63 John Bocco akiwa na kipa aliteleza na kipa kuuwahi na kuudaka.

Kipre Tchetche aliiandikia Azam bao la pili, baada ya kukokota mpira na kumfunga tela beki wa Simba,Adam Miraji aliyeshindwa kumkaba na kumhadaa kipa Dhaira na kupiga mpira uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Omari Mngindo anaripoti kutoka Uwanja wa Mabatini, Chalinze kwamba Ruvu Shooting na Kagera zimetoka sare ya bao 1-1.
Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo katika Uwanja huo ambapo, Yanga itachuana na Mgambo Shooting Tanga.

Nayo Coastal Union iliichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga

No comments: