MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe (CHADEMA), amesema anawashangaa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kumuweka kitimoto baada ya kuanika viwango vya mishahara ya viongozi.
Hivi karibuni akiwa kwenye ziara ya
kuimarisha chama chake Kanda ya Magharibi, Zitto alitaja viwango vya mishahara
wanayolipwa wabunge, mawaziri, waziri mkuu na rais.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi
eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Zitto alisema kuwa aliwashangaa
wabunge wa CCM kumuweka kitimoto kuhusu jambo hilo wakiwa kwenye kamati za
Bunge.
“Niliwaambia kwamba mbona hata
mshahara wa Rais wa Marekani, Barack Obama, umewekwa mitandaoni ukionesha
analipwa dola 400,000?” alihoji.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu
wa CHADEMA, alihoji ni kwanini viongozi wa hapa nchini hawapendi kuwaeleza
wananchi mishahara wanayopata, ukiwamo wa rais anayelipwa sh milioni 384 kwa
mwaka.
“Nilipoingia Ofisi Ndogo za Bunge
juzi, baadhi ya wabunge walianza kunishambulia kwa maneno wakitaka kujua sababu
za kutaja mshahara wa rais.
“Niliwauliza kwani kuna tatizo gani
kuutaja wakati amechaguliwa na wananchi na hiyo fedha anayolipwa ni kodi yao?
Nikawahoji, pale Ikulu kuna kazi ngumu anayofanya?” alisema.
Zitto aliongeza kuwa rais anasafiri,
anavalishwa, anakula bure kwa fedha za wananchi, sasa kwa nini mshahara wake
wasiujue, na kwa nini usikatwe kodi.
Aliongeza kuwa sababu ya kutaja
mishahara ya viongozi wa juu wa serikali ni kuwaeleza wananchi wajue ukweli
ndipo wapate hasira pindi wanapocheleweshewa maendeleo katika maeneo yao.
Zitto aliongeza kuwa wabunge
wanalipwa mshahara wa sh milioni 11.2 kwa mwezi kwa kazi ya kuzungumza pekee,
huku posho ikiwa ni sh 330,000 kila siku.
“Mambo kama hayo ni lazima wananchi
wayajue na ndiyo maana wabunge hawataki yajulikane, kwa sababu wananchi
wakiyafahamu watawabana wawajibike katika nafasi zao,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya
Katiba mpya, Zitto aliwalaumu wabunge wa CCM kwa kutokuwa na nia ya kupatikana
kwa katiba hiyo kutokana na mizengwe waliyomfanyia Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wakishirikiana na Naibu Spika, Job Ndugai.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya
Chang’ombe, Edith Bunjoro, maarufu kama Mama Kevin, aliwataka wananchi wa kata
hiyo kumuunga mkono katika juhudi zake za kulikomboa jimbo hilo kutoka mikononi
mwa CCM.
No comments:
Post a Comment