Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa
kivita (ICC) hii leo imetoa masharti kwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuhusu
kuhudhuria vikao vya kesi dhidi yake katika mahakama hiyo kuanzia Novemba 12
mwaka huu.
Hii inafuatia ombi la Rais Kenyatta
kutaka kuruhusiwa kutohudhuria vikao vya kesi dhidi yake kutokana na majukumu
yake kama Rais wa Kenya.
Kati ya majaji watatu wanaosikiliza
kesi dhidi ya Kenyatta wawili walikubali kumruhusu kutohudhuria kesi dhidi yake
huku jaji anayeongoza kesi hiyo Kuniko Ozaki akipinga ombi la Kenyatta.
Hata hivyo Kenyatta ametakiwa kuwepo
mahakamani kwa ufunguzi wote wa kesi dhidi yake, hotuba za ufunguzi wa pande
zote husika , kusikiliza maoni ya waathiriwa na wasiwasi wao , uamuzi
utakapotolewa na vikao vyovyote atakavyotakiwa na majaji kuhudhuria.
Ikiwa itawezekana Kenyatta pia
atatakiwa kuhudhuria kikao cha uamuzi wa kesi yake.
Iliamuliwa kuwa ikiwa Rais Kenyatta
atakosa kutii masharti hayo , basi huenda majaji nao wakamuondolea faida hizo
na kutolewa kwa kibali cha kumkamata.
Naibu Rais Ruto pia amepata afueni
hiyo ila kwa masharti yaliyotolewa kwa Kenyatta ili kuwawezesha kuendelea na
majukumu yao kama viongozi wa nchi.
Majaji pia wamesema wameamua kutoa
masharti haya kwa Kenyatta ili kutoonekana kuwa na mapendeleo dhidi ya Kenyatta
na kuonyesha heshima kwa haki za mshukiwa lakini pia kuwalinda waathiriwa na
mashahidi katika kesi hiyo.
Rais Kenyatta amekuwa akiitaka
mahakama ya ICC kumruhusu kutohudhuria kesi yake kutokana na majukumu yake kama
Rais wa Kenya.
Ombi hili liliwasilishwa kupitia kwa
Muungano wa Afrika ambao ulisema kuwa utawasilisha malalamiko yake kwa baraza
la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mahakama ICC inatumika kuwakandamiza
viongozi wa Afrika.
Muungano huo ulimshauri Kenyatta na
naibu wake kutohudhuria kesi zao kwani wao ni viongozi wa nchi na wanapaswa
kuruhusiwa kuendelea na majukumu yao kama viongozi wa Kenya.
Cha zaidi AU ilitaka kesi dhidi ya
Kenyatta kuahirishwa kwa mwaka mmoja. Kenyatta na Ruto wanatuhumiwa kwa
kuongoza ghasia za kikabila zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007/2008
ambapo zaidi ya watu elfu moja walifariki.
Chanzo: BBCswahili
No comments:
Post a Comment