Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac),Zitto Kabwe PICHA |MAKTABA
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac),Zitto Kabwe amevilipua vyama vya
siasa kwa uvunjaji wa sheria na kusimamisha ruzuku ya kila mwezi hadi
vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za umma tangu mwaka 2009 kwa
Msajili wa Vyama vya Siasa.
Pia kamati hiyo itawaweka kitimoto
makatibu wakuu wa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku ili wajieleze ni kwa nini hawajawasilisha
taarifa hiyo hadi sasa.
Alisema hayo jana wakati kamati hiyo
ilipokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa katika Ofisi ndogo za Bunge.
Zitto alisema tangu mwaka 2009 vyama
tisa vya siasa vinavyopewa ruzuku na Serikali vilipata jumla ya Sh67.7 bilioni
lakini havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa msajili kama
vinavyopaswa kufanya hivyo kisheria.
“Ninaagiza msajili kuanzia sasa
ruzuku isitolewe kwa chama chochote cha siasa hadi hapo kitakapowasilisha
ripoti ya ukaguzi wa hesabu tangu mwaka 2009 hadi sasa na makatibu wataitwa ili
wajieleze kwa nini hawajafanya hivyo,” alisema.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa,
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alipoulizwa jana alisema: “Ninahitaji muda
kuangalia kama kweli taarifa hiyo haijawasilishwa na sheria inasemaje kuhusu
suala hilo,” alisema.
Alisema baada ya siku mbili za kazi
atakuwa na majibu ya kuridhisha kuhusiana na suala hilo.
Viongozi wengine wa vyama vya siasa
vinavyopata ruzuku, hawakupatikana kuelezea hali hiyo. Zitto aliongeza,“ Hivi
ni vyama vya siasa ambavyo wakati ukifika vinaweza kuja kuongoza Serikali,
lakini inashangaza ni kwa nini vinatumia fedha za walipakodi bila kukaguliwa,
huu ni uvunjaji wa sheria.”
Kwa mujibu wa Zitto, vyama hivyo na
fedha za ruzuku walizopata kwenye mabano tangu mwaka 2009 ni CCM (Sh50.9
bilioni), Chadema (Sh9.2 bilioni) na CUF (Sh 6 bilioni).
Vingine ni NCCR-Mageuzi(Sh677
milioni),UDP (Sh333 milioni), TLP (Sh217 milioni), APPT-Maendeleo (Sh217
milioni), DP (Sh3.3 milioni) na Chausta (Sh2.2 milioni).
Zitto alisema ingawa jukumu la
ukaguzi wa fedha za umma ni la ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali lakini hakufanya hivyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Alisema vyama vya siasa viliagizwa
kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi kama vilivyokuwa vikifanya zamani
hadi hapo ofisi ya CAG itakapopata fedha.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa
msajili kuviagiza vyama vya siasa kutenga sehemu ya fedha za ruzuku kwa ajili
ya ukaguzi.
Alisema viongozi hao waone kwamba
suala la ukaguzi wa fedha za ruzuku ni muhimu ili kuleta uwazi katika matumizi
ya fedha za umma.
“Sasa kamati imeshindwa kuendelea na
kazi kwa sababu hakuna hesabu zilizokaguliwa, nendeni tutawaita siku nyingine,”
alisema.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema vyama hivyo vimekuwa vikidai kwamba havina
ruzuku ya kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi.
“Kwa hiyo siwezi kuchukua fedha
nikavipa vyama vya siasa kwaajili ya ukaguzi wakati hazijatengwa katika
bajeti,” alisema.
Hata hivyo,Zitto alimwelekeza Mutungi
kwamba fedha za ukaguzi ziko kwenye ruzuku wanazopewa na kwamba hiyo siyo
sababu ya kuhalalishwa kutokaguliwa kwa hesabu zao.
No comments:
Post a Comment