Dar/Iringa. Rais Jakaya Kikwete
amesema maadui wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania
kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali
yake itaendelea kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka
kuvuruga nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Kulikuwapo na upepo mbaya,
lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais Kikwete
jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru,
mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni,
maadui wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi,
lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na nchi iko
salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali
haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba
nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za
maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni
mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu
yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba
Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama
ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania
itasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na
kuwarudishia Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya
Muungano wetu. Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo
ili historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine
baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya
miaka hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema
Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa
mchakato wa kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja
umoja wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba
itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais
Kikwete.
Alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho
ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa kwa mwaka huu ni kusisitiza mshikamano wa
kitaifa unaopinga mbinu zozote za kuligawa taifa. “Kaulimbiu ya mwaka huu;
Tanzania ni wamoja, tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini, itikadi,
rangi au rasilimali,” alisema Rais Kikwete.
Alisisitiza kuwa amekusudia
mabadiliko ya Katiba ambayo mchakato wake unaendelea yawe ya kulipeleka mbele
taifa kimaendeleo kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete
alisema atapendelea kuona Katiba Mpya inazinduliwa Aprili 13, mwakani, siku
ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa Baba wa Taifa.
Alisema kitendo hicho kitaienzi zaidi
siku hiyo na kuandamana na mpango wa kubadilisha maadhimisho ya kitaifa ya
kumkumbuka Mwalimu Nyerere kutoka Oktoba 14 siku aliyofariki na kuwa Aprili 13,
siku aliyozaliwa.
..ataka kuvuruga Mwenge
Maadhimisho ya Mwenge nusura yaingie
dosari baada ya mwanamume kujichomeka katika kundi la wanahabari akiwa na lengo
la kumdhuru kiongozi wa Mbio za Mwenge.
Kitendo hicho kilifanyika wakati Rais
Kikwete akiwa tayari ameshuka chini katika jukwaa dogo akisubiri kukabidhiwa mwenge
huo, mtu huyo alichomoka kutoka katika kundi la waandishi wa habari na kujaribu
kumvamia kiongozi wa Mbio za Mwenge, Juma Ali Sima aliyekuwa ameshikilia Mwenge
huo.
Hata hivyo, jitihada za mtu huyo za
kutaka kumvamia kiongozi wa Mwenge zilikwama baada ya kudhibitiwa vikali na
askari waliokuwa wakilinda amani uwanjani hapo.
Katika kipindi hicho, Rais Kikwete
pamoja na wasaidizi wake wengine walikuwa mita kama tisa kutoka katika eneo la
tukio akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo.
Rais Kikwete alisema kilele cha
maadhimisho ya Mbio za Mwenge kimefanywa kuwa pia siku ya kumbukumbu ya Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.
Alisema Watanzania wote bila kujali
vyama vyao wana wajibu wa kuyakumbuka mema yote ya Mwalimu Julius Nyerere ikiwa
ni pamoja na mafundisho yake.
Rais pia alisema ili kumkumbuka zaidi
Mwalimu Nyerere alipendekeza siku yake ya kuzaliwa ndiyo iitwe Nyerere Day na
ianze kusherehekewa kwa mbwembwe, iwe na mijadala ya kazi zake na itumiwe
kufanya shughuli mbalimbali za kujenga taifa kwa lengo la kumuenzi.
Kuhusu dawa za kulevya
Katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alizungumzia mkakati
wa Serikali yake wa kupambana na dawa za kulevya kwamba kitaanzishwa chombo
maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kazi ya kupambana na dawa za kulevya ni ngumu na
hatari kutokana na wanaofanya kazi hiyo kuwa na fedha nyingi, lakini Serikali
itawalinda wote.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment