Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Suala la kuendelea na muundo wa sasa
wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) au kulifumua na kuliunda upya, imekuwa
hadithi ya muda mrefu ambayo imesikika kwenye jamii yetu kiasi cha kuonekana
kuwachosha wengi. Hata Rais Jakaya Kikwete alipokuwa ziarani nchini Marekani hivi
karibuni aliirudia hadithi hiyo kwamba Serikali ina mpango wa kulifumua shirika
hilo ili liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Akizungumza jijini New York na ujumbe
wa Shirika la Millenium Challenge (MCC), linalofadhili miradi mbalimbali hapa
nchini, ikiwamo nishati, Rais Kikwete alisema marekebisho hayo, ambayo alisema
yamepewa kipaumbele yanalenga kuisaidia Serikali kuharakisha jitihada zake za
kusambaza umeme kwa watu wengi zaidi. Kama sote tujuavyo, Tanesco kwa muda wote
wa maisha yake, ndilo limekuwa shirika pekee linalozalisha, kusambaza na kuuza
nishati hiyo nchini.
Tunaikaribisha ahadi hiyo ya Rais
Kikwete lakini kwa hadhari kubwa, kwani ni mwendelezo wa hadithi ambazo amekuwa
akizitoa waziri wake wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Kwa mara
ya mwisho waziri huyo aliliambia Bunge la Bajeti mjini Dodoma kwamba kutokana
na utendaji mbovu na kushamiri kwa vitendo vya rushwa, Tanesco ingevunjwa na
kuundwa kampuni mbili au tatu.
Ndiyo maana tunasema hadithi hizo ni
za muda mrefu na zimewachosha wananchi wengi wanaohitaji nishati ya umeme ambao
wameendelea kuteseka kwa sababu ya muundo mbovu wa shirika hilo na vitendo vya
ufisadi.
Muundo huo kwa miongo mingi ndiyo
umekuwa chanzo au sababu ya urasimu, umangimeza na hata wizi usio na kipimo
ambao umelididimiza shirika hilo na kuwa tegemezi kwa Serikali. Tunafahamu
kuwa, Tanesco ilianzishwa kisheria kwa majukumu ya msingi ya kufua, kusambaza
na kuuza umeme kutokana na mahitaji yaliyokuwapo wakati ule. Hivi sasa mambo
yamebadilika kutokana na mahitaji ya nishati hiyo kuongezeka maradufu. Hivyo,
majukumu matatu ya msingi ya Tanesco hayana budi kutenganishwa.
Tunashauri sheria mpya itungwe,
iruhusu ushindani kama ambavyo imefanyika kwenye sekta nyingine, ikiwamo ya
mawasiliano. Tunadhani kwamba ushindani na mafanikio yanayopatikana kwenye
kampuni za simu ukipelekwa Tanesco utasaidia kuwapa wananchi huduma nzuri na
hatimaye kurejesha imani kwa shirika hilo.
Licha ya kushusha gharama, ushindani
pia utaongeza idadi ya wateja kutoka idadi ya sasa ambayo tunaambiwa ni chini
ya asilimia 20 ya wananchi wote wanaotumia umeme huo wa Tanesco.
Hata hivyo, wasiwasi wetu ni kuwa,
kutungwa kwa sheria hiyo mpya bila kuruhusu ushindani haitakuwa na maana
yoyote, badala yake itaendeleza mfumo wa mashirika ya umma na idara za Serikali
kuendelea kuwa wadeni wakubwa wa shirika hilo.
Tunapenda kuiona sheria mpya
ikiwabana wezi wa umeme na kuwashughulikia kama ilivyo kwa wezi wengine, kwani
wizi na ubadhirifu ni kosa la jinai.
Ni kwa msingi huo tunashauri Sheria
ya Umeme, Namba 10 ya Mwaka 2008 ifanyiwe marekebisho ili iondoe mazingira
yanayoruhusu ukiritimba, kwa maana ya kutoa uhuru kwa wazalishaji wadogo wa
umeme kuuza nishati hiyo kwenye soko huria badala ya Tanesco pekee. Tunashauri
pia miradi iliyo chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), isilazimishwe
kuingizwa Tanesco ili gharama za umeme zisiendelee kupaa.
No comments:
Post a Comment